Michezo

Chepng’etich ange kuhifadhi ubingwa wa mbio za mita 1,500 duniani

October 5th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

FAITH Chepng’etich Kipyegon na Winny Chebet wataelekezewa macho ya karibu hii leo Jumamosi watakaposhuka ulingoni kwa nia ya kunyakulia Kenya medali katika fainali ya kivumbi cha mita 1,500 kwa upande wa wanawake jijini Doha, Qatar.

Chepng’etich atakuwa akilenga kutetea taji ambalo alilizoa mnamo 2017 Riadha za Dunia zilipoandaliwa jijini London, Uingereza.

Malkia huyu alitawazwa bingwa wa Riadha za Diamond League mnamo 2017 baada ya kushinda fainali jijini Brussels, Ubelgiji na kutuzwa kombe la almasi na kima cha Sh5.5 milioni. Alikosa taji la Diamond League mnamo 2016 alipomaliza fainali katika nafasi ya saba na kupoteza tuzo ya Sh4.5 milioni.

Mnamo 2017, Chepng’etich alimduwaza kwa mara nyingine mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za mita 1,500 kwa upande wa wanawake, Genzebe Dibaba wa Ethiopia na kutwaa medali ya dhahabu jijini London.

Chepng’etich ambaye aliibuka bingwa wa Jumuiya ya Madola mnamo 2014, pia alijitwalia medali ya dhahabu katika mbio hizo za mizunguko mitatu uwanjani katika mashindano ya Olimpiki ya 2016 yaliyofanyika jijini Rio, Brazil.

Chepng’etich ndiye mtimkaji wa pekee aliyeaminiwa kuyabeba matumaini yote ya Kenya ya kupata medali katika mbio hizo za wanawake baada ya wenzake waliopigiwa upatu wa kutamba, Winny Chebet na Judy Kiyeng kubanduliwa mapema mnamo 2017. Aliwapiku kwa urahisi washindani wake wengine wakuu katika mzunguko wa mwisho, wakiwemo Laura Muir (4: 02.97, Uingereza), Sifan Hassan (4: 03.34, Uholanzi) na Laura Weightman (4:04.11, Uingereza).

Dibaba alilazimika kuridhika na nafasi ya 12 kwa muda wa dakika 4:06.72 wakati huo. Simpson ambaye aliishindia USA medali ya pili katika mbio hizo baada ya kutwaa shaba katika Olimpiki za 2016 jijini Rio, Brazil aliongeza kasi ikiwa imesalia mizunguko miwili na kuwapiku Laura na Caster Semenya wa Afrika Kusini ambaye alipigiwa upatu wa kutia kapuni nishani ya dhahabu. Laura Weightman ambaye ni mshikilizi wa rekodi ya mbio hizo katika taifa lake la Uingereza alizidiwa maarifa na kuambulia nafasi ya sita kwa kutumia muda wa dakika 4: 04.11.

Katika mchujo wake Jumatano wiki hii, Chepng’etich aliambulia nafasi ya pili kwa muda wa dakika 4:03.93 nyuma ya Mholanzi Sifan Hassan (4:03.88) ambaye alijizolea nishani ya dhahabu katika mbio za mita 10,000 mwishoni mwa wiki iliyopita. Kwa upande wake, Chebet pia alikamilisha mchujo wa kundi lake katika nafasi ya pili kwa muda wa dakika 4:08.36 nyuma ya Rababe Arafi wa Morocco ambaye anatazamiwa kuwatatiza mno.

Wanaridha wengine watakaonogesha fainali za leo Jumamosi katika mbio hizo za mita 1,500 kwa upande wa wanawake ni Winnie Nanyondo (Uganda), Nikki Hiltz (Amerika), Shelby Houlihan (Amerika), Laura Muir (Uingereza), Ciara Mageean (Ireland), Gudaf Tsegay (Ethiopia) na Gabriela DeBues Stafford wa Canada.