Chepng’etich arejea mbio za nyika kwa kishindo, alenga kutawala Riadha za Dunia nchini Hungary

Chepng’etich arejea mbio za nyika kwa kishindo, alenga kutawala Riadha za Dunia nchini Hungary

Na GEOFFREY ANENE

MALKIA wa Olimpiki na dunia mbio za mita 1,500, Faith Chepng’etich alirejea kwa kishindo katika mbio za nyika baada ya kutwaa taji la Sirikwa Classic uwanjani Lobo Village, Eldoret.

Chepng’etich,29, ambaye mara ya mwisho alikuwa ametimka mbio hizo ni 2017 wakati wa Mbio za Nyika duniani mjini Kampala, Uganda, alitawala kitengo cha wanawake kilomita 10 kwa dakika 33:50 baada ya kudhibiti mbio kutoka mzunguko wa tatu.

Bingwa wa Jumuiya ya Madola na Riadha za Dunia za watimkaji wasiozidi umri wa miaka 20 mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji Jackline Chepkoech aliridhika na nafasi ya pili kwa 34:52 naye mshindi wa medali ya dhahabu ya Riadha za Dunia za watimkaji wasiozidi umri wa miaka 20 mita 3,000 Zenah Jemutai akafunga tatu-bora kwa 35:08 mbele ya mashabiki 10,000.

“Huu ni mwanzo wa msimu wangu ninapotumai kuwa na msimu mzuri katika mbio za uwanjani. Nalenga kushinda taji langu la tatu la dunia uwanjani,” alisema  Chepng’etich na kufichua kuwa hakutarajia kabisa kupata ushindi.

Riadha za Dunia zitafanyika Agosti 17-29 mjini Budapest, Hungary. Mzawa wa Kenya  Roselida Jepketer kutoka Bahrain alikamata nafasi ya nne (35:13).

Charles Lokir aliendelea kupata umaarufu aliponyakua taji la wanaume kilomita 10, wiki chache baada ya kushinda mbio za nyika za kitaifa mjini Nairobi.

“Nimekuwa na msimu mzuri wa mbio za nyika na hiyo inanipatia nafasi nzuri kabla ya msimu wa riadha za uwanjani ambapo natumai kufanya vyema katika 10,000m na kupata tiketi ya Riadha za Dunia,” alisema Lokir,22.

Alibeba taji kwa dakika 30:14, mwaka mmoja baada ya kuwa nambari tano Sirikwa Classic na nambari tisa wakati wa mashindano ya kuchagua timu itakayoshiriki Mbio za Nyika duniani nchini Australia mwezi Machi. Josphat Kiprotich alikamata nafasi ya 30:19 naye Dennis Kipng’etich akawa wa tatu 30:26).

Bingwa wa kitaifa mbio za nyika za wanaume wasiozidi umri wa miaka 20 Samuel Kibathi na Lucy Nduta kutoka Nyahururu walishinda vitengo vya chipukizi.

  • Tags

You can share this post!

Mallorca yaduwaza Real Madrid katika pambano la La Liga

Barcelona wakomoa Sevilla na kufungua mwanya wa alama nane...

T L