Michezo

Chepng’etich, Barsoton kuongoza Wakenya mbio za Delhi

November 12th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

Malkia wa mbio za kilomita 42 kwenye Riadha za Dunia za mwaka 2019 Ruth Chepng’etich anaongoza orodha ya Wakenya watakaowania taji la Airtel Delhi Half Marathon nchini India hapo Novemba 29.

Katika orodha ya washiriki iliyotangazwa na Shirikisho la Riadha Duniani hapo Novemba 11, Chepng’etich atashirikiana na Evaline Chirchir, Brillian Kipkoech na Eva Cherono katika kitengo cha wanawake ambacho hakuna Mkenya ameshinda tangu Cynthia Limo aibuke bingwa mwaka 2015.

Leonard Barsoton, Josphat Boit na Edwin Kiptoo ni wawaniaji wa taji la kitengo cha wanaume ambacho Kenya ina ukame wa miaka mitatu.

Waethiopia wametawala makala matatu mfululizo yaliyopita ya wanaume yakiwemo mawili yaliopita kupitia kwa Andamlak Belihu. Pia, wameng’aria wapinzani katika makala manne mfululizo ya wanawake yakiwemo mawili yaliyopita kupitia kwa Tsehay Gemechu.

Wakenya bado wanatarajiwa kupata kibarua kigumu kutoka kwa Ethiopia ambayo katika kitengo cha wanawake inawakilishwa na watimkaji wakali Gemechu anayeshikilia rekodi ya Delhi Half Marathon (saa 1:06:00) pamoja na chipukizi matata Yalemzerf Yehualaw aliyekamilisha makala yaliyopita katika nafasi ya pili, na bingwa wa mbio za kilomita 21 duniani mwaka 2018 Netsanet Gudeta.

Ushindani mkali katika kitengo cha wanaume utatoka kwa Waethiopia Belihu pamoja na Guye Adola na Amdework Walelegn wanaojivunia kasi ya juu kuliko washiriki wengine.

Mshikilizi wa rekodi ya Bara Asia ya nusu-marathon Abraham Cherobei kutoka Bahrain pia hawezi kupuuzwa katika vita hivyo ambavyo washindi wa vitengo hivyo watazawadiwa Sh2.9 milioni.

Wakenya ambao wamewahi kutwaa mataji ya Delhi Half Marathon ni Philip Rugut (2005), Francis Kibiwott, Lineth Chepkurui (2006), Mary Keitany (2009), Geoffrey Mutai (2010), Lucy Kabuu (2011), Edwin Kipyego (2012), Florence Kiplagat (2013 na 2014), Cynthia Limo (2015) na Eliud Kipchoge (2016).