Cherargei akashifu Uhuru baada ya wanariadha waliowasili kutoka Japan kupata mapokezi baridi

Cherargei akashifu Uhuru baada ya wanariadha waliowasili kutoka Japan kupata mapokezi baridi

Na CHARLES WASONGA

SENETA wa Kaunti ya Nandi Samson Cherargei amemlaumu Rais Uhuru Kenyatta na serikali kwa ujumla kufuatia kile anachotaja kama mapokezi duni ya wanariadha nyota wa Kenya walipowasili nchini kutoka Japan, Jumatano usiku.

Akiongea na wanahabari katika majengo ya bunge, Alhamisi, Bw Cherargei alilalamika vikali kwamba hakuna afisa wa cheo cha juu serikalini aliyefika kuwalaki wanariadha hao wakiongozwa na nyota wa mbio za kilomita 42 (Marathon), Eliud Kipchoge.

“Ni aibu kwamba Rais wetu Uhuru Kenyatta alikuwa akikutana na viongozi wa kikabila Mombasa badala ya kuwapokea wanariadha wetu waliovuna medali katika mashindano ya Olimpiki jijini Tokyo, Japan. Isitoshe, bingwa Eliud Kipchoge hakupata mapokezi kutoka kwa Waziri wa Michezo Amina Mohamed na maafisa wa Kamati ya Olimpiki Nchini (NOCK),” akalalamika.

Bw Cherargei alisema tofauti na wanariadha wa Uganda waliozoa medali na waliopokelewa kama mashujaa huku Rais wa nchini hiyo Yoweri Museveni akiwatunuku magari ya kifahari, Kipchoge na wenzake walitunukiwa “shuke ya Kimaasai” pekee.

“Japo shuka ya Kimaasai ni kitambulisho chetu kama Wakenya. Nadhani wanariadha wetu walifaa kupewa zawadi nzuri walipowasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta. Ni aibu kuwa huku wenzao wa Uganda wakipewa magari ya kisasa – SUV – wetu hawakupewa chochote,” akaeleza.

Seneta wa Nandi Samson Cherargei analalamikia mapokezi duni ya nyota wa Olimpiki wa Team Kenya. Hapa ni majengo ya bunge, Agosti 12, 2021. Picha/ Charles Wasonga

Hata hivyo, kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, msemaji wa serikali Cyrus Oguna alisema kuwa maafisa wakuu wa serikali hawakuwapokea wanariadha wa Kenya katika uwanja wa JKIA, kama njia ya kuzuia msambao wa Covid-19.

You can share this post!

Rekodi nyingine katika soka ya Uingereza baada ya Chelsea...

Pigo kwa Arsenal baada ya Sheffield United kumkwamilia kipa...