Habari

Cherargei apokonywa wadhifa wa mwenyekiti kamati ya seneti kuhusu sheria

May 26th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SENETA wa Kaunti ya Nandi Samson Cherargei apokonywa wadhifa wa Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Sheria.

Seneta wa Laikipia John Kinyua ametimuliwa kutoka Uenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Ugatuzi.

Na Seneta wa Kaunti ya Bomet Langat Christopher Andrew amepokonywa cheo cha Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu.

Haya ni baadhi ya mabadiliko ambayo yametangazwa na kiranja wa wengi Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata.

Mabadiliko hayo yatawasilishwa rasmi katika kikao cha Seneti saa nane na nusu leo Jumanne.

Naye Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju ametangaza kuwa Mkutano wa Baraza Kuu (NEC) utafanyika “wakati wowote kuanzia Alhamisi wiki hii” kuidhinisha mabadiliko ya uongozi wa Jubilee katika Bunge la Kitaifa.

“Baada ya mkutano wa NEC kutakuwa na mkutano wa Kundi la Wabunge baadaye kupitisha mabadiliko hayo, ” akasema Bw Tuju kwenye kikao na wanahabari katika makao makuu ya chama hicho.

Wakati huo huo, maseneta watano waliosusia mkutano wa Ikulu wamefika mbele ya kamati ya nidhamu kujitetea.

Waliofika ni Millicent Omanga, Falhada Dekow, Victor Prengei, Mary Seneta na Naomi Waqo.

Tuju amesema hatima yao sasa itaamuliwa na kamati hiyo inayoongozwa na wakili Lumatete Muchai.

Ametetea mabadiliko ya uongozi chamani yaliyofanywa katika bunge la seneti siku kadhaa zilizopita.

Amefafanua kwamba operesheni hiyo ililenga kuleta nidhamu chamani na kamwe “haiwezekani chama kiwe na viongozi wasioheshimu chama na kiongozi wake”.

Tuju aidha amesema chama tawala cha Jubilee kitaweza kuendeleza mikakati yake hasa ya maendeleo kwa Wakenya ikiwa wanachama wake watadumisha nidhamu na ahadi walizotoa kabla wachaguliwe.

“Kama chama kinachotawala hatuwezi kupiga hatua bila nidhamu. Yeyote yule katika chama lazima awe na nidhamu, atii chama na kiongozi wake,” Bw Tuju akaambia wanahabari.

Maseneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet), Prof Kithure Kindiki (Tharaka Nithi) na Susan Kihika (Nakuru), waliondolewa katika nyadhifa zao; kiongozi wa wengi, naibu kiongozi wa wengi na kiranja katika seneti, mtawalia.

Ni mabadiliko yanayoonekana kulenga wandani wa Naibu Rais Dkt William Ruto chini ya kundi la ‘Tangatanga’.

Wengi wa waliounga mkono mabadiliko hayo wanaegemea kundi la ‘Kieleweke’ linalounga mkono Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, kupitia muafaka kati yao kuunganisha taifa; handisheki.

Mnamo Jumanne, katibu wa Jubilee hata hivyo amesema mabadiliko hayo yalitekelezwa kwa mujibu wa sheria za chama.

“Tunahakikishia Wakenya kuwa hatua tutakazochukulia watovu zitafuata mkondo wa sheria,” akasema.

Katika bunge la seneti, JP tayari imetangaza mabadiliko ya kamati mbalimbali. Mjeledi huo wa nidhamu unatarajiwa kuelekezwa katika bunge la kitaifa.