Habari

Cherargei asema maseneta wengi hawakujua chochote kuhusu mkutano wa Ikulu

May 13th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

VIONGOZI wanaoegemea mrengo unaomuunga mkono Naibu Rais William Ruto wameendelea kutoa hisia mseto kuhusu mabadiliko ya uongozi wa Jubilee (JP) katika bunge la seneti yaliyofanywa Jumatatu katika Ikulu ya Rais, Nairobi.

Spika wa bunge hilo Ken Lusaka Jumanne aliidhinisha kuteuliwa kwa seneta wa Pokot Magharibi Samuel Poghisio (Kanu) kama kiongozi wa wengi, wadhifa ulioshikiliwa na Seneta wa Elgeyo Marakwet Kiphumba Murkomen (JP) ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto.

Mabadiliko mengine aliyotia muhuri spika Lusaka, ni uteuzi wa Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata wa Jubilee kama kiranja, wadhifa uliokuwa wa Seneta wa Nakuru Susan Kihika (JP) mshirika wa karibu wa naibu rais.

Mkutano wa Ikulu kufanya mabadiliko hayo, ulihudhuriwa na maseneta wanaomuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta, ingawa orodha ya majina yao haijawekwa paruwanja. Naibu Rais Dkt Ruto hakuhudhuria, maseneta wanaoegemea upande wake wakidai hawakupokea mwaliko.

Seneta wa Nandi Samson Cherargei amesema Jumatano wengi walifahamu kuhusu mkutano huo wa Ikulu kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.

“Nilidhani walialikwa kwa kikombe cha chai na mandazi,” seneta huyo amesema.

Bw Cherargei amesema hakupokea mwaliko wowote kuhudhuria mkutano huo, sawa na maseneta wengine.

Akikosoa mabadiliko hayo, seneta huyo amesema sheria za chama hazikufuatwa.

Licha ya spika Lusaka wakati akipitisha mageuzi hayo kwenye kikao cha bunge kudai maseneta 20 ndio waliyapitisha, Cherargei amesema chama cha Jubilee kina maseneta 34 na kwamba 22 hawakuhudhuria mkutano wa Ikulu.

“Mabadiliko hujiri kwa utaratibu na kufuata sheria. Hawakufuata sheria kwa sababu walijua hawana idadi kuyatekeleza,” amesema akitaka picha za mkutano huo ziwekwe wazi.

Amesema waliobanduliwa walikuwa wameteuliwa na chama ila si ‘watu binafsi’.