Cherera afeli kufika mwenyewe mbele ya JLAC

Cherera afeli kufika mwenyewe mbele ya JLAC

NA CHARLES WASONGA

NAIBU mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Juliana Cherera Jumatatu, Novemba 28, 2022, alifeli kufika mbele ya Kamati ya Bunge Kuhusu Haki na Masuala ya Kitaifa (JLAC) inayosikiliza ombi la kutimuliwa kwake.

Badala yake, Cherera, ambaye alitarajiwa kujitetea mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Tharaka George Murugara, alituma wakili wake Apollo Mboya.

Wabunge wanachama wa kamati hiyo, wakiongozwa na mwenyekiti George Murugara walimtaka Bw Mboya kutangaza ikiwa mteja wake, Cherera, umekubali kwamba JLAC ina mamlaka ya kikatiba kusikiliza suala hilo, kabla ya yeye kuwasilisha utetezi wake.

“Kabla ya kikao hiki kuendelea tungetaka kujua ikiwa sasa anakubali kwamba kamati hii ina mamlaka ya kisheria kusikiliza maombi kutoka kwa walalamishi hao wanne. Hii ni kwa sababu mnamo Alhamisi, Novemba 24 wiki jana, wewe na mawakili wengine wa washtakiwa mliondoka kutoka kikao cha kamati hii mkidai kuwa JLAC haina mamlaka ya kusikiliza maombi ya kutimuliwa kwa wateja wenu. Je, umebadilisha msimamo au ungali unashikilia msimamo wa wiki jana?” Bw Murugara ambaye ni Mbunge wa Tharaka, akauliza.

Kauli ya mwenyekiti huyo iliungwa mkono na kiranja wa wengi Silvanus Osoro, John Makali (Kanduyi), Njeri Maina (Mbunge Mwakilishi wa Kirinyaga) miongoni mwa wengine.

Hata hivyo, Bw Mboya alishikilia kuwa suala hilo la mamlaka ya JLAC liibuliwa wiki jana na mwenyekiti Bw Murugara akatoa uamuzi.

“Suala hili liliibuliwa wiki jana na mwenyekiti akatoa uamuzi wake kwayo. Kwa hivyo, leo siwezi kurejelea suala hilo hapa,” Bw Mboya akasema.

Hata hivyo, wakili huyo alilalamika kwamba stakabadhi na rekodi za nukuu za kamati hiyo (Hansard Records) ambazo aliomba Karani wa Bunge Samuel Njoroge ampe hazikuwa zimetumwa kwake ili azikague kabla ya kuwasilisha utetezi wake.

Ni kwa misingi hiyo ambapo kamati hiyo ilikubali kuahirisha kikao cha kusikiza utetezi kutoka kwa upande wa Bi Cherera hadi Jumanne, Novemba 29, 2022, saa mbili za asubuhi.

Wakenya wanne wamewasilisha maombi ya kutoka bunge kupitia Kamati ya JLAC ipendekeze kutimuliwa kwa Bi Cherera na makamishna Justus Nyang’aya, Irene Masit na Francis Wanderi.

Wanadai kuwa kutaa matokeo ya uchaguzi wa urais yaliyotangazwa na mwenyekiti Wafula Chebukati mnamo Agosti 15, walitaka kutumbukiza taifa hili katika machafuko.

  • Tags

You can share this post!

TALANTA: Dogo nguli wa Afrobeat

BENSON MATHEKA: Usalama wa kila mtahiniwa uhakikishwe...

T L