Cherera naye ajiuzulu na kuacha Raila hoi

Cherera naye ajiuzulu na kuacha Raila hoi

NA LEONARD ONYANGO

WANDANI wa Rais William Ruto sasa wanataka kinara wa Azimio la Umoja Raila Odinga azuiliwe kuandaa mkutano kesho Jumatano kupinga serikali.

Wanasema kujiuzulu kwa naibu mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Juliana Cherera kumefanya maandamano yanayopangwa na Bw Odinga kukosa mashiko.

Bi Cherera alijiuzulu jana siku mbili baada ya Rais Ruto kuunda jopo la kumchunguza pamoja na makamishna wenzake; Francis Wanderi, Irene Masit na Justus Nyang’aya.

Rais Ruto anashutumu wanne hao kuunda njama ya kumnyima ushindi katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Makamishna hao walijitenga na matokeo ya urais yaliyotangazwa na mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati huku wakitaka ushindi wa Rais Ruto kubatilishwa.

Rais Ruto aliwasimamisha kazi kwa muda makamishna hao na kisha kuunda jopo la kuwachunguza baada ya Bunge kupendekeza watimuliwe.

Rais Ruto aliteua Jaji wa Mahakama Kuu Aggrey Muchelule kuongoza jopo la kuwachunguza makamishna hao. Wanajopo wengine ni Carolyne Kamende Daudi, Linda Gakii Kiome, Mathew Njaramba Nyabena, Kanali (Mstaafu) Saeed Khamis Saeed.

Jopo hilo linafaa kuwachunguza makamishna hao na kuwasilisha mapendekezo yake kwa Rais kufikia Januari 2023.

“Nilitekeleza majukumu yangu kama kamishna wa IEBC kwa bidii na uadilifu. Hata hivyo, hatua niliyochukua kwa nia njema imechukuliwa na kufasiriwa vibaya,” akasema Bi Cherera katika barua yake ya kujiuzulu.

Akaongeza: “Baada ya kutafakari kwa umakini matukio ya hivi karibuni ndani ya IEBC na kushauriana na familia yangu pamoja na mawakili wangu, nimekubali kwamba hakuna haja ya kuendelea kuwa kamishna. Nimeamua kujiuzulu.”

Kamishna Nyang’aya alikuwa wa kwanza kujiuzulu Ijumaa saa chache baada ya Rais Ruto kuunda jopo hilo.Kujiuzulu kwa Bw Nyang’aya na Bi Cherera kunamaanisha kuwa jopo hilo litahoji makamishna wawili tu – Bw Wanderi na Bi Masit.

Bw Odinga ameshikilia kuwa kuhangaishwa kwa makamishna hao ‘waasi’ ni miongoni mwa sababu kuu zinazomfanya kuongoza mapambano dhidi ya serikali.

Sababu nyingine zinazomfanya Bw Odinga ‘kukosana’ na Rais Ruto ni ‘kutimuliwa’ kwa Makatibu wa Wizara waliokuwa wameteuliwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, hatua ya serikali kukosa kutoa mikopo ya Hustler Fund isiyokuwa na riba kama alivyoahidi wakati wa kampeni kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, ‘kupendelea’ baadhi ya jamii katika uteuzi serikalini na mpango wa kutaka kuagiza magunia milioni 10 ya mahindi yaliyobadilishwa maumbile (GMO) kutoka ughaibuni.

Lakini Seneta wa Nandi Samson Cherargei jana Jumatatu aliitaka serikali kuzuia Bw Odinga kufanya mkutano au maandamano ya kupigania makamishna hao wanne huku akisema kuwa kujiuzulu kwao kumefanya mpango wa Bw Odinga kuisha nguvu kisiasa.

“Kujiuzulu kwa makamishna wawili wa IEBC kumeweka Bw Odinga njiapanda. Alilenga kutumia kisingizio cha makamishna hao kuandamana. Serikali inafaa kumnyima kibali cha kufanya mkutano,” akasema Bw Cherargei.

Naye, naibu Spika wa Bunge la Kitaifa Gladys Shollei alitaka jopo la Jaji Muchelule kuendelea na shughuli yake hata kama makamishna wanaofaa kuchunguzwa watajiuzulu wote.

Rais Ruto jana Jumatatu alishauri viongozi kwenda kortini kupeleka malalamishi yao dhidi ya serikali. Lakini aliyekuwa mwaniaji mwenza wa urais wa Azimio la Umoja Bi Martha Karua alipuuzilia mbali ushauri huo.

Bi Karua alishikilia kuwa mkutano wa kesho uwanjani Kamkunji, Nairobi, utafanyika ‘na hakuna yeyote atakayezuia hata agizo la mahakama tutapuuza’.

Bi Karua alisema kuwa upinzani utaandaa sherehe mbadala za Jamhuri Desemba 12 katika uwanja wa Jacaranda.

Kwa upande wake Bw Odinga alisema kuwa mkutano wake wa kesho uwanjani Kamkunji utakuwa wa amani na wala si maandamano.

“Hatutashiriki katika vurugu au uharibifu wa mali. Serikali isitumie kisingizio hicho kuchochea vurugu,” akasema Bw Odinga.

Bw Odinga jana alipata nguvu baada ya chama cha Jubilee kusema kuwa kitashiriki katika mikutano ya kupinga serikali.

Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni alisema kuwa atawasiliana na Bw Odinga ili apewe ratiba ya mikutano hiyo.

You can share this post!

Aliyehukumiwa kifungo cha miaka 28 kwa mauaji awa huru

TSC yasifu walimu kujitolea kisiwani

T L