NA BENSON MATHEKA
KIONGOZI wa Azimio la Umoja-One Kenya, Raila Odinga ameapa kwamba hatakubali makamishna wanne wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mpaka (IEBC) waliosimamishwa kazi kwa kupinga matokeo ya kura ya urais Agosti 9 waondolewe ofisini.
Bw Odinga alisisitiza kuwa serikali ya Kenya Kwanza inawaandama makamishna hao ikilenga uchaguzi mkuu ujao wa 2027 na kutaja hatua hiyo kama hatari kwa demokrasia nchini.
Kwenye taarifa kali baada ya Rais William Ruto kuteua jopo la kuwachunguza makamishna hao, Naibu Mwenyekiti Juliana Cherera, Irene Masit, Francis Wanderi na Justus Nyang’aya (aliyejiuzulu jana Ijumaa), Bw Odinga alisema hatakubali nchi kurudi katika enzi za matumizi mabaya ya katiba na sheria.
Kujiuzulu kwa Nyang’aya kutamwepushia kufika mbele ya jopo hilo lakini huenda kukamkosesha kiinua mgongo anachostahili kupewa iwapo angehitimisha muhula wake wa kuhudumu katika tume hiyo.
Rais Ruto aliteua jopo litakalosimamiwa na Jaji Aggrey Muchelule aliyeapishwa jana Ijumaa na Jaji Mkuu Martha Koome pamoja na wanachama wengine; Carolyne Kamende Daudi, Linda Gakii Kiome, Mathew Njaramba Nyabena, Kanali mstaafu Saeed Khamis Saeed, Emmanuel Kibet Kirui na Irene Tunta Nchoe.
Wakili wa jopo hilo ni Peter Munge Murage atakayesaidiwa na Zamzam Abdi Abib.
Akizungumza baada ya kuhudhuria mkutano wa viongozi wa mashanani Nairobi jana, Bw Odinga alitaja kusimamishwa kwa makamishna hao kama udikteta na njama ya kuiba uchaguzi mkuu wa 2027.
“Azimio haitaketi na kuruhusu serikali iwaondoe makamishna hao ofisini. Tunataka kumkumbusha Bw Ruto kwamba nchi hii ilikuwa na mfumo kama anaojaribu kurudisha. Tulipiga vita mfumo huo. Tuliuporomosha mfumo huo. Tutafanya hivyo tena,” Bw Odinga alisema akionekana kurai wafuasi wake kujitokeza.
“Tuungane tupiganie nchi yetu kabla ya mambo kuharibika,.” alisema.
Waziri huyo mkuu wa zamani alisisitiza kuwa ataongoza wafuasi wake kwa mkutano wa umma katika uwanja wa kihistoria wa Kamukunji, Nairobi hapo Jumatano Desemba 7.
Bw Odinga alisema kwamba mkutano huo na mingine atakayoandaa katika ngome za upinzani ni ya kushauriana kuhusu mwelekeo ambao nchi inachukua chini ya serikali ya Rais William Ruto.
Katika hatua inayoweza kuzua makabiliano na serikali, Bw Odinga alitangaza kuwa atafanya mkutano mwingine katika uwanja wa Kamukunji siku ya Jamhuri Dei, Desemba 12.
“Siku ya Desemba 7, tutazindua mikutano ya umma ya mashauriano katika uwanja wa kihistoria wa Kamukunji. Na tutarudi katika uwanja huo tena Desemba 12 kuendelea na mashauriano,” alisema.
Hata hivyo, baadhi ya vyama tanzu vya Azimio vimejitenga na mikutano hiyo.
Bw Odinga alisisitiza kuwa hataacha uamuzi wa serikali kuwatimua makamishna hao kuendelea bila kupingwa akisema kuwa ni sehemu ya njama za serikali ya Kenya Kwanza kubomoa demokrasia.
Jamhuri Dei ni Siku Kuu ya Kitaifa na Rais William Ruto anatarajiwa kuongoza sherehe za kitaifa katika Bustani ya Uhuru Park.
Hii inaweza kusababisha polisi kupiga marufuku mkutano wa Raila katika uwanja wa Kamukunji.
Bw Odinga alikataa mswada unaolenga kubadilisha mchakato wa kuajiri makamisha wa IEBC ambao Kenya Kwanza inapanga kuwasilisha bungeni akisema ni hatua ya kupanga wizi wa kura katika uchaguzi mkuu ujao.
Subscribe our newsletter to stay updated