Cherono sasa alenga taji la Dunia, Madola

Cherono sasa alenga taji la Dunia, Madola

MFALME mpya wa Valencia Marathon Lawrence Cherono sasa ametupia jicho mataji makubwa ya Riadha za Dunia na Jumuiya ya Madola mwaka 2022.

Cherono aliwasili nyumbani kutoka Uhispania mapema jana na kupokelewa kishujaa na rafiki na jamaa wake katika uwanja wa ndege wa Eldoret katika Kaunti ya Uasin Gishu.Mwanariadha huyo alinyakua taji la Valencia Marathon katika jaribio lake la pili kwa saa 2:05:12, sekunde 0.04 mbele ya Muethiopia Chalu Deso (2:05:16).

Naye Mkenya Philemon Kacheran akaridhika na nafasi ya tatu (2:05:19).Mkenya Nancy Jelagat alitawala kitengo cha kinadada kwa 2:19:31 akifuatiwa na Waethiopia Woldu Etagegne (2:20:16) na Degefa Beyenu (2:23:04).Mfalme mara mbili wa New York Marathon, Geoffrey Kamworor, ambaye alikuwa akirejea baada ya karibu miaka miwili kutokana na jeraha, alikamata nafasi ya nne (2:05:23).

Cherono alisema ushindi wake ni wa kumfariji mtimkaji wa marathon na jirani wake Philip, aliyepoteza mkewe akijifungua pacha siku chache kabla ya Cherono kuelekea Valencia.Cherono alifurahia kukamilisha msimu kwa kishindo akiongeza kuwa atafurahi zaidi kujumuishwa katika timu ya Kenya ya Riadha za Dunia mjini Eugene, Amerika, na Jumuiya ya Madola mjini Birmingham, Uingereza, mwezi Agosti.

Ushindi wa Cherono mjini Valencia ulipatikana miezi minne baada ya kumaliza Olimpiki 2020 katika nafasi ya nne mjini Sapporo, Japan. Alisema hapo jana kuwa baada ya Olimpiki, alimakinikia mazoezi ya Valencia Marathon na anafurahia mazoezi hayo yalizaa matunda.

“Nashukuru makocha na wanariadha ninaofanya nao mazoezi kwa sababu maandalizi baada ya Olimpiki yalikuwa mafupi sana,’ alisema. Aidha, mabingwa wa Olimpiki Eliud Kipchoge na Faith Chepng’etich wametiwa katika orodha ya watu sita wanaowania tuzo ya mwanamichezo bora wa Bara Afrika wa Shirika la Utangazaji la BBC.

Kura zinapigwa hadi Desemba 19 kabla ya mshindi kujulikana Januari 7, 2022.

You can share this post!

Koth Biro mechi mbili kuchezwa Alhamisi

Masumbwi ya Jamal yang’oa nanga Kisumu

T L