Michezo

Cheruiyot ahifadhi taji lake Riadha za Diamond League

July 13th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

TIMOTHY Cheruiyot ni Mkenya pekee aliyekuwa na siku nzuri kwenye duru ya Monaco ya Riadha za Diamond League baada ya kuhifadhi taji lake kwa dakika 3:29.97.

Cheruiyot, ambaye mwaka 2019 ameshinda pia duru za Stockholm (Uswidi), Stanford (Marekani), Lausanne (Uswizi) na kumaliza nambari mbili katika duru ya kufungua msimu jijini Doha nchini Qatar, alifuatwa kwa karibu na raia wa Norway Jakob Ingebrigtsen (3:30.47) na Mganda Ronald Musagala (3:30.58).

Wakenya wengine walioshiriki mbio hizi za mizunguko mitatu ni George Manangoi, Charles Simotwo, Vincent Kibet, Brimin Kiprono na Michael Kibet, ambao walimaliza katika nafasi za sita, tisa, 10, 13 na 14, mtawalia.

Nao Ferguson Rotich (mita 800) na Benjamin Kigen (mita 3,000 kuruka viunzi na maji) walimaliza vitengo vyao katika nafasi ya pili nyuma ya Nijel Amos (Botswana) na Soufiane El Bakkali (Morocco) mtawalia, huku Nelly Jepkosgei aliyekuwa Mkenya pekee katika mbio za mita 800 za wanawake, akivuta mkia.

Nusura rekodi ivunjwe

Rekodi ya dunia ya David Rudisha ya mbio za mita 800 ya dakika 1:40.91 iliponea kidogo kuvunjwa baada ya Mbotswana Amos kumaliza sekunde 58 nje yake.

Alitwaa taji kwa dakika 1:41.89, muda ambao ni kasi ya juu tangu Rudisha aweke rekodi ya dunia mwaka 2012.