Michezo

Cheruiyot apeperusha bendera Kenya ikipata matokeo mseto tenisi nchini Morocco

August 24th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KENYA iliandikisha matokeo mseto Ijumaa katika tenisi ya mchezaji mmoja kwa mmoja kwenye michezo ya Bara Afrika (African Games) inayoendelea nchini Morocco.

Kevin Cheruiyot alimbwaga Mamadouba Makadji kutoka Guinea kwa seti mbili bila jibu za alama 6-0, 6-0 saa chache baada ya Mkenya mwenzake Ibrahim Kibet kuonyeshwa kivumbi.

Kibet alinyamazishwa kwa seti mbili kavu za alama 6-4, 6-2. Cheruiyot sasa atashiriki raundi ya 16-bora itakayoanza Jumapili.

Wakenya wengine wanaoshiriki tenisi ya mchezaji mmoja kwa mmoja ya wanaume ni Ismael Changawa aliyeratibiwa kumenyana na Mtunisia Mohamed Dougaz naye Albert Njogu akabiliane na Bernard Alipoe-Tchotchodji kutoka Togo baadaye Jumamosi.

Akina dada wanaopeperusha bendera ya Kenya katika tenisi ni Angela Okutoyi, Alicia Owegi, Judith Nkata na Faith Omurunga.

Mbali na tenisi, Kenya pia inashiriki riadha, ambayo itaanza kesho, badminton, voliboli ya ufukweni, ndondi, judo, karate, uogeleaji, taekwondo, handboli, tenisi ya meza, mpira wa vikapu wa wachezaji watatu kwa watatu, mchezo wa kupiga makasia, triathlon, voliboli, uendeshaji wa baiskeli na ulengaji shabaha.

Tukienda mitamboni, Kenya ilikuwa imezoa medali nne ambzo ni ya shaba kutoka mwendeshaji baiskeli Nancy Akinyi na katika taekwondo kupitia Everlyne Aluoch katika uzani wa kati ya kilo 67 na kilo 73.

Wanavoliboli ya ufukweni Gaudencia Makokha na Naomi Too walinyakua nishani ya fedha naye Faith Wanjiku akazoa medali nyingine ya fedha katika taekwondo uzani wa zaidi ya kilo 73.