Michezo

Cheruiyot atangazia Dunia yeye mfalme mbio za mita 1,500

October 8th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

TIMOTHY Cheruiyot alithibitishia ulimwengu kuwa ufanisi aliopata katika msimu wa kawaida kwenye Riadha za Diamond League haukuwa wa kubahatisha pale aliponyakua medali ya dhahabu katika mbio za mita 1,500 jijini Doha, Qatar, Jumapili usiku.

Cheruiyot, ambaye mwaka huu alijishindia taji la tatu mfululizo kwenye Diamond League, aliteremka Doha akipigiwa upatu kutwaa taji baada ya kutawala duru ya Stockholm (Uswidi), Stanford (Amerika), Lausanne (Uswisi), Monaco na Brussels (Ubelgiji) na kuandikisha kasi ya juu ya dakika 3:28.77 mjini Lausanne.

Alidhihirisha uweledi huu alipoongoza kitengo hiki cha kuzunguka uwanja mara tatu kutoka mwanzo hadi mwisho.

Alitwaa taji kwa dakika 3:29.26, sekunde mbili mbele ya bingwa wa Olimpiki mwaka 2012 Taoufik Makhloufi kutoka Algeria (3:31.38). Marcin Lewandowski aliridhika na medali ya shaba kwa rekodi mpya ya Poland ya dakika 3:31.46.

Cheruiyot aliongoza mizunguko miwili ya kwanza akiwa na Ronald Kwemoi, lakini Mkenya huyo mwenzake akashindwa kustahimili kasi ya juu. Kengele ilipolia, Cheruiyot alikuwa amefungua mwanya wa mita 25 kati yake na wakimbiaji wengine, na ingawa alianza kukaribiwa katika kona ya mwisho, alikwamilia uongozi na kunyakua medali yake ya kwanza kabisa ya dhahabu.

Katika mashindano makubwa ya awali, Cheruiyot alizoa nishani ya fedha kwenye Riadha za Afrika mwaka 2016 na 2018, Riadha za Dunia mwaka 2017 na Jumuiya ya Madola mwaka 2018.

Ushindi waendeleza utawala

Ushindi wa Cheruiyot uliendeleza utawala wa Kenya katika mbio za mita 1,500 kwenye Riadha za Dunia hadi makala matano.

Asbel Kiprop alishinda makala ya mwaka 2011 (Korea Kusini), 2013 (Urusi) na 2015 (China) naye Elijah Manangoi akatamba mwaka 2017 nchini Uingereza.

Manangoi hakutetea taji kutokana na jeraha la kifundo.

“Nilihisi niko sawa kabisa mbio zilipoanza kwa sababu mimi hufanya mazoezi makali na pia nilitaka kuepuka kusukumana na kugongana na mtu. Ulikuwa mpango wangu kukibia jinsi nilivyofanya. Nashukuru Mungu nilifanya vyema kutoka mwanzo hadi mwisho na ninafurahia kuwa mshindi. Msimu wa Olimpiki unakaribia kwa hivyo nitaendelea kuongeza bidii,” alisema Cheruiyot baada ya ushindi.