Michezo

Cheruiyot na Mo Farah watikisa Great North Run

September 10th, 2018 1 min read

Na Geoffrey Anene

VIVIAN Cheruiyot alijishindia taji lake la pili tangu mwaka 2016 katika mbio za Great North Run baada ya kuongoza Wakenya Brigid Kosgei, Joyciline Jepkosgei na Linet Masai kufagia nafasi nne za kwanza mjini Newcastle nchini Uingereza, Septemba 9, 2018.

Bingwa wa Paris Marathon mwaka 2018 Betsy Saina hakuwa na bahati aliposalimu amri katika kilomita ya 15.

Mkenya mwingine Daniel Wanjiru, ambaye aliibuka mfalme wa mbio za London Marathon mwaka 2017, alikamilisha kitengo cha wanaume katika nafasi ya saba, huku Muingereza Mo Farah akiendelea kutawala mbio hizi tangu mwaka 2014 kwa kunyakua taji.

Jake Robertson kutoka New Zealand, ambaye mwaka 2017 alizuzua mashabiki kwa kupiga goti baada ya kukamilisha mbio hizi na kuomba Mkenya Magdalyne Masai amuoe, aliridhika katika nafasi ya pili naye Mbelgiji Bashiri Abdi akafunga tatu-bora.

Makala ya mwaka huu yalivutia washiriki 50, 000 wakiwemo wakimbiaji 550 watajika.