Michezo

Chesi: Chipukizi Robert Mcligeyo aingia katika kikosi cha timu ya taifa

February 20th, 2024 2 min read

NA TOTO AREGE

MCHEZAJI chipukizi wa mchezo wa chesi Robert Mcligeyo kwa mara ya pili mfululizo, amefanikiwa kuingia kwenye kikosi cha taifa kama mchezaji bora.

Uteuzi wa mwisho wa timu ya taifa ulikamilika mwishoni mwa wiki jana, katika KCB Club jijini Nairobi, huku Mcligeyo, mwenye umri wa miaka 18, akiongoza kitengo cha Open kwa alama nane kutokana raundi 11.

Bingwa wa sasa wa taifa wa wanawake Sasha Mongeli aliongoza upande wa wanawake kwa alama 7.5.

Katika makundi yote mawili, wachezaji bora 11 wa ndani walipambania nafasi tano za juu za timu ya taifa.

Wachezaji hawa sasa watawakilisha  taifa katika mashindano ya yajayo ya kimataifa baadae mwaka huu, ikiwa ni pamoja na Olimpiki ya Chess yenye hadhi kubwa.

Olimpiki ya Chesi itafanyika Budapest, Hungary kuanzia Septemba 10 hadi Septemba 23, 2024.

Mbali na Mcligeyo ambaye ana alama 2041, wachezaji wengine walioshindana katika kitengo cha Open ni pamoja na bingwa wa Chesi wa Kitaifa wa Kenya (KNCC) Joseph Methu (1990), mabingwa wa zamani Martin Njoroge (1896), Mehul Gohil (2020) na Victor Ngani (1939), mchezaji wa sifa tele Kenneth Omolo (2066), Ian Matuge (1782), Matthew Kamau (1939), Elvis Likoko (1875), Lenny Mataiga (1847), na Kinoti Mutuma (1540).

Katika kitengo cha Wanawake, Mongeli (1763), bingwa wa zamani wa kitaifa na Mwalimu wa Wanawake Joyce Nyaruai (1797), Bingwa wa Chess wa Wanawake Chipukizi wa Dunia wa 2021 Chini ya -1700 Glenda Madelta (1522), Jully Mutisya (1560), Nicole Albright (1431), Mercy Ingado (1292), Ether Karanja (1354), Wanjiru Kimani (1403), Eliabeth Kassidy (1436), Zuri Kaloki (1285) na Yvonne Adego (1160).

Isipokuwa Mcligeyo, Methu, Mongeli na Nyaruai, wachezaji wengine walipata tiketi ya moja kwa moja kuingia raundi ya pili ya mchujo kutokana na uzoefu wao.

“Nimefurahi jinsi mambo yalivyokwenda kwa sababu awali, sikuwa nimepanga kucheza kwani ninaelekeza nguvu zangu kwa Michezo ya Afrika mwezi ujao nchini Ghana. Mashindano yalikuwa magumu kuliko mwaka 2023,” alisema Mcligeyo.

Katika kitengo cha wanawake, Nicole na Ingado ni wachezaji wapya waliopata nafasi kwenye timu ya taifa.

Nicole ambaye hajafanikiwa katika majaribio kadhaa alimaliza wa tatu na alama 6.5. Ingado ambaye ni bingwa wa Taifa wa Vijana wa chini ya miaka 18 pia alipata alama 6.5.

Wachezaji wa timu ya Taifa ya Chess ya Kenya 2024

Kitengo cha Open

  1. Robert Mcligeyo
  2. Martin Njoroge
  3. Ian Mutuge
  4. Matthew Kamau
  5. Elvis Likoko

Kitengo cha Wanawake

  1. Sasha Mongeli
  2. Jully Mutisya
  3. Albright Nicole
  4. Mercy Ingado
  5. Joyce Nyaruai