Michezo

Chiesa aondoka Juventus kuchezea Liverpool


LIVERPOOL imemsajili wing’a matata Federico Chiesa kwa Sh1.6 bilioni katika mkataba ambao una kipengele cha staa huyo kupata nyongeza ya Sh500 milioni iwapo ujio wake kikosini utaifanya Liverpool kuimarika zaidi.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 amesaini mkataba wa miaka minne baada ya kuagana na vigogo wa Italia, Juventus.

Staa huyo wa timu ya taifa ya Italia ndiye mchezaji wa kwanza mpya kusaili Anfield tangu kocha Arne Slot achukuwe usukani kutoka kwa Jurgen Klopp aliyeondoka baada ya msimu kumalizika.

Chiesa alikuwa katika kikosi cha Italia kilichoshinda Uingereza kupitia kwa mikwaju ya matuta kwenye fainali ya Euro 2020 ugani Wembley.

“Nimefurahia mno kujiunga na klabu hii kubwa yenye sifa za kujivunia. Richard Hughes aliponipigia simu aliuliza, ‘uko tayari kujiunga na Liverpool? – na kocha akanipigia tena- na jibu lango lilikuwa. Niko tayari kabisa kwa sababu naelewa historia ya klabu hii, na mahitaji ya mashabiki wake,’ Chiesa alisema kupitia kwa akaunti ya mtandao wa kijamii ya Liverpool. “Nimefurahia, na niko tayari kabisa kuanza kazi.”