Habari Mseto

Chifu anaswa akimumunya hongo

June 7th, 2020 1 min read

NA CHARLES WANYORO

Maafisa wa upelelezi kutoka Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) walimkamata chifu mmoja katika Kaunti ya Meru kwa kumumunya hongo ili asuluhishe mgogoro kati ya majirani wawili.

Maafisa hao kutoka kaskazini mwa Kenya walimkamata chifu huyo wa Mbeu Joshua Karithi aliyedaiwa kuwa alipokea pesa kutoka kwa Edward Mutie ambaye ana mgogoro na jiraniye.

Mkuu wa EACC eneo hilo George Ojowi alisema kwamba kesi hiyo imekuwa ikisitishwa kwa mwaka mmoja sasa kwasababu Bw Mutie alikuwa ameagizwa kulipa 3,000 pesa ambazo hangemudu kuzilipa.

Mlalamishi alisema kwamba chifu huyo alikuwa amemuomba alipe Sh600 ili amsaindie kutatua shida yake na jirani yake lakini wakasikizana Sh300, fedha ambazo alipewa na EACC. Hapo ndipo chifu huyo alikamatwa akipokea pesa hizo za mtego huku akirekodiwa.

“Alikamatwa pamoja na Bw Isiah Miriti na Peter Mugambi na tukachukua pesa zetu kutoka mifukoni mwa washukiwa hao.  EACC imehakikisha kwamba video na mawasiliano waliyo nayo yanaonyesha jinsi maaafisa hao huchukua hongo na baadaye kugawana pesa hizo za mtego,” alisema Bw Ojowi.