Habari Mseto

Chifu anayehusishwa na kifo cha mwanafunzi aachiliwa


NAIBU chifu wa Kijiji cha Amabuko, Kisii, Bw Simon Osano, anayetajwa kuhusika katika kifo cha mwanafunzi wa kidato cha kwanza aliyejitoa uhai kwa kunywa sumu amekamatwa.

Kamanda wa Polisi Kaunti Ndogo ya Masaba Kusini, Robert Kibuchi alithibitisha kukamatwa kwa afisa huyo, akidokeza kwamba ameandikisha taarifa na polisi.

“Alirekodi taarifa yake lakini baadaye aliachiliwa kwa dhamana ya kibinafsi. Uchunguzi unaendelea,” Bw Kibuchi aliambia Taifa Dijitali kwa njia ya simu.

Msimamizi huyo ambaye amekuwa ofisini kwa muda wa wiki moja tu, amejikuta matatani baada ya kudaiwa kumpiga viboko mwanafunzi huyo kwa kutokwenda shule.

Wazazi wa msichana huyo ndio waliokuwa wamemripoti.

Marehemu alikunywa sumu baada ya kukerwa na uamuzi wa chifu kumwadhibu mbele ya babake na wazee wengine.

Lakini kabla ya kutekeleza kitendo hicho, aliacha barua ambapo alimlaumu afisa huyo wa serikali kwa kumdhalilisha.

“Nimeamua kumfuata Yesu. Kwa hayo yote umenitendea, uzidi kubarikiwa. Sasa umenichapa mbele ya baba, mjomba na watu wengine,” inasema sehemu ya barua hiyo inayodaiwa kuandikwa na mwanafunzi huyo.

Aliandika barua hiyo kwa mchanganyiko wa lugha za Ekegusii, Kiingereza na Kiswahili.

Mwanafunzi huyo alikuwa mama wa mtoto mmoja na alimwomba msimamizi huyo amlelee mtoto wake.

Pia, alimuagiza afisa huyo kuhakikisha anahudhuria mazishi yake na kuwasihi waombolezaji wengine wahudhurie safari yake ya mwisho ulimwenguni kwa wingi.

“Acha barua hii ikufikie popote ulipo. Hakikisha unahudhuria maziko yangu. Sio matakwa yangu kujiua na mimi sio wa kwanza kufa. Mtunze mtoto wangu, nakuomba sana,” aliongeza.

Marehemu aliandika barua hiyo yenye kichwa, “Barua kwa chifu wetu Simion Osano.”

Marehemu alifichua kwamba alivumilia masaibu ya kutisha na aibu kubwa katika afisi ya naibu chifu alipokuwa akiadhibiwa.

Alidai aliitwa kila aina ya majina na kuambiwa kwamba alikuwa na hamu ya kuzuru nyumba za wavulana.

Marehemu aliongeza kuwa waadhibu wake walifikia kiwango cha kutumia gugu moja linalowasha ili ahisi uchungu zaidi.

Alimuaga mtoto wake na kufanya toba kwa Muumba wake.

“Mwanangu naomba ubaki na amani. Nitameza sumu ambayo nitainunua kwa sababu nilizoeleza. Nakuombea uishi miaka mingi. Mimi sio wa kwanza kufa,” marehemu aliongeza.

Kulingana na ripoti za matibabu katika hospitali ya Keroka ambapo mwathiriwa alikimbizwa, marehemu alikunywa sumu mnamo Alhamisi, Julai 4, 2024 na kufariki Jumamosi, Julai 6.

Mwili wake umehifadhiwa katika hospitali hiyo ukingoja upasuaji.

Mwendazake alifichua nambari yake ya siri ya kufikia pesa za simu maarufu kama M-Pesa.