Habari MsetoMakala

Chifu anayekabili uasherati, HIV kwa kutandika wazinifu mijeledi

February 16th, 2020 4 min read

Na BERNARD OJWANG

KAUNTI ya Homa Bay imegonga vichwa vya habari mara nyingi kwa sababu zisizo njema kama vile kukithiri kwa maambuizi ya HIV, mimba za mapema na kadhalika.

Lakini sasa, chifu mmoja katika kaunti hiyo ameamua kudumisha nidhamu kwa kukabiliana na uasherati katika eneo lake kwa njia ya kipekee.

Chifu Bob Odhiambo wa lokesheni ya Arujo, humchapa viboko mtu yeyote anayepatikana akifanya mapenzi hadharani, anayepatikana akizini ama yeyote anayedhulumu mtoto kimapenzi.

Anaamini kuwa hatua hiyo itasaidia kukabili maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi.

Ripoti ya hivi punde kabisa kutoka kwenye Baraza la Kukabili Ukimwi Nchini ilisema kuwa Kaunti ya Homa Bay inaongoza katika maambukizi mapya ya virusi hivyo.

Takwimu zinaonyesha kuwa wanawake ndio wanaathiriwa zaidi, wakiwa ni asilimia 21.1 huku asimilia 19 ya wanaume ikiwa imeathiriwa.

Utafiti umebainisha kwamba usherati unachangia pakubwa ueneaji wa maambukizi hayo kwa kasi.

Jitihada kadhaa zimefanywa kukabili mtindo huu lakini mbinu hii ni muhali.

Kila asubuhi, Bw Lang’o huamka kujitayarisha kwa siku iliyo mbele yake na katika masuala ya familia.

Nyumbani kwake, ni wazi jinsi yeye ni kielelezo kwani mapenzi na uwiano wa kifamilia ni bayana kwa mgeni yeyote anayewatembelea.

Anasema ni nidhamu hii anayoitaka miongoni mwa wakazi wa kata ya Arujo.

Katika mahojiano, alisema aliamua kuchukua hatua ya kuchapa viboko washerati kwa sababu alikuwa akipokea ripoti kila siku kuhusu watu wanaozini.

Bw Odhiambo aliamua kunyoosha tabia za wakazi katika eneo lake.

“Tumegundua kwamba wanaume ndio huhusika zaidi katika uasherati. Ijapokuwa inasemekana wanawake wamekuwa wakiwanyima wanaume haki zao, hiyo si sababu ya watu kujihusisha katika uasherati. Lazima turudishe nidhamu. Sitaki uasherati katika kata yangu,” akasema.

Alieleza jinsi hali imekuwa mbaya hadi watu hushiriki ngono hadharani bila kujali, huku wanawake wakongwe pia wakinyemelea vijana wadogo.

“Juzi kuna mama alikuja kwangu akaniambia kuna mama mzee anajamiiana na kijana wake. Nilimwita nikamtwanga kwelikweli! Watoto wa shule wanafaa kuachwa wasome,” akasema.

Wakazi wa kata hiyo wamesifu hatua za chifu wao na kusema imesaidia sana kudumisha ndoa na kuepusha watu kuhatarisha maisha yao kwa magonjwa ya zinaa.

Mkazi Samwel Omondi alisema tangu chifu huyo alipoanza kuchapa watu viboko, nidhamu imeanza kurejea katika eneo hilo na uasherati umepungua.

“Hapa ilikuwa mambo ni usherati kila mahali. Ukitembea kwa kichochoro unakuta tu mwanamke amekamatwa na bwana ya mtu…mwanamume na bibi ya mtu, hata watoto wa shule. Hali ilikuwa mbaya sana na usherati ilikuwa juu. Tangu chifu aanze kutumia viboko, kuna heshima sasa,” akasema Bw Omondi.

Mkazi mwingine, Bi Beatrice Akinyi alieleza jinsi wanaume walianza kutoa vijisababu visivyo na msingi walipokuwa wakiulizwa kwa nini wanajihusisha katika usherati ilhali wameacha wake zao nyumbani.

“Hata unapowauliza kuhusu kile kinawafanya watoke, hawasemi. Wanatoa tu maneno yasiyo na msingi…mara kusema kwamba hawapati chakula. Acha kiboko iendelee,” akasema Bi Akinyi.

Chifu Odhiambo anaogopwa na wengi. Anaamini kuwa anachokifanya kitasaidia kuzuia kusambaa kwa virusi vya Ukimwi.

Kulingana naye, idadi ya walio na Ukimwi katika eneo hilo ni ya kutamausha, ndiposa anawaadhibu wasiozingatia maadili.

Anasema kuwa hajali iwapo kuna watu wanamchukia kwa misimamo yake, bora lengo lake liafikiwe.

“Hata wakinichukia au la, mimi sijali. Heshima lazima idumu na ugonjwa wa Ukimwi pia upungue,” akasema chifu huyo.

Juhudi zake zimeleta tabasamu katika nyuso za baadhi ya vijana walio kwenye ndoa.

Bi Pamela Adoyo ni mmoja wa walionufaika kwa kiboko cha chifu.

Anasema alikuwa na ndoa yenye misukosuko lakini baada ya kuripoti kwa chifu, sasa ana furaha.

“Zamani nilikuwa naishi maisha mabaya. Mume wangu alikuwa analala nje, tunalala njaa na watoto. Yeye mara ameenda na bibi ya mtu mwingine kwa lojing’i, akirudi ananipiga vibaya. Nilienda kwa kanisa ili niombe lakini hilo halikusaidia,” akasema.

Bi Adoyo alichukua hatua na kwenda kwa chifu wa micharazo ndipo akapata usaidizi.

“Nakwambia alichapwa mbele yangu kwelikweli. Hadi wa leo tunaishi kwa amani. Ikifika saa kumi na mbili jioni unakuta asharudi kwa nyumba akiwa amebebea familia kitu kwa mkoba. Chifu amenisaidia,” akasema.

Bi Elizabeth Akoth mwenye umri wa miaka 47 pia alimshukuru Chifu Odhiambo kwa kumsaidia. Anadai kuwa uzinzi ulikuwa umeathiri ndoa yake pakubwa lakini sasa mambo yameimarika.

“Mimi nilikuwa napigwa. Maisha yangu yalikuwa magumu sana. Tangu anyoroshwe, mambo sasa yako safi. Ameniheshimu,” akasema.

Katika kitongoji cha Shauri Yako, kata ya Arujo mkazi Collince Olang, anasema ngono za kiholela zilikuwa jambo la kawaida hapa.

Bw Olang ambaye alikiri pia alikuwa akijihusisha na tabia hiyo, kwa sasa amefungua ukurasa mpya maishani.

“Tulikuwa tunaelekea pale Sofia (kituo cha kibiashara). Ukiona bibi ya mtu amevaa nguo imemshika mwili vizuri, unachukua namba yake kisha unampa Sh200…mambo kwisha,” anaeleza.

Chifu Odhiambo anasema kuwa, kituo hicho cha kibiashara kilikuwa mojawapo ya maeneo sugu zaidi ya usherati.

“Nilienda huko nikapata kila kitu kimesambaratika. Katika uwanja kulikuwa na watu wanalala na wake au mabwana za watu. Nilitwanga kweli kweli! Ilikuwa ni aibu sana kila mahali ukigeuka ni mipira ya kondomu. Kuna wengine wengi walikuwa wakitenda usherati bila kutumia kinga. Ilikuwa ni Sodoma na Gomora,” akasema.

Bw Olang anakumbuka kilichofanyika mwaka jana baada ya sherehe za siku ya Jamhuri.

Alijiunga na rafiki yake katika uwanja wa Homa Bay kama kawaida, kuwasubiri wanawake wanaoenda sokoni na kuwapa Sh200 ili wakubali kulala nao.

Walishikwa papo hapo na chifu Odhiambo wakirushana roho. Viboko alivyovipokea vilibadilisha maisha yake.

Inadaiwa kuwa chifu aliwawekea mtego baada ya kupashwa habari na wakaazi wenye ghadhabu.

“Hapo kulikuwa kubaya. Ukishamalizana na huyu unatafuta mwingine, na saa hizo huyo ni bibi ya mtu,” akasema Bw Olang.

Bw Olang sasa ni mwingi wa toba. Kwa sasa anashirikiana na chifu kukabiliana na ngono za kiholela. Anasaidia chifu kufika maeneo yote ambako usherati umekuwa ukifanyika.

“Kwa wenye nililala na mabibi zao naomba msamaha, sikujua. Saa hizi naunga chifu mkono na hii tabia lazima tumalize,” akasema.

Wakaazi wa hapa, haswa kina mama walioolewa, wamepongeza sana juhudi za chifu Odhiambo.