Chifu asimamishwa kazi kwa kutafuna hongo ya Sh30,000

Chifu asimamishwa kazi kwa kutafuna hongo ya Sh30,000

Na RICHARD MUNGUTI

NAIBU wa chifu katika kata ya Highridge, Nairobi Jumatatu aliagizwa asimamishwe kazi mara moja baada ya kushtakiwa kwa kula mlungula wa Sh30,000 kutoka kwa mfanyabiashara.

Hakimu mwandamizi Bw Felix Kombo aliamuru Bw Justus Atieri Malunda akome kufanyakazi ya umma hadi kesi aliyoshtakiwa ya ufisadi itakaposikizwa na kuamuliwa.

“Kwa mujibu wa sheria za ufisadi mtumishi wa umme akishtakiwa anakoma mara moja kuhudumu hadi mahakama itakapoamua hatma yake,” Bw Kombo alimweleza Bw Malunda.

Hakimu huyo aliamuru afisi ya mkurugenzi wa umma (DPP) iwasilishe kortini barua ya kusimamishwa kazini kwa Bw Malunda katika muda wa wiki mbili.

Bw Kombo alimweleza mshtakiwa kuwa sheria za ufisadi zilifanyiwa marekebisho na kuwataka watumishi wote wa umma wakishtakiwa wakome mara moja kutoa huduma kwa umma.

Bw Malunda alikabiliwa na shtaka la kumwitisha Bw Mela Singh na mkewe Mandeep Channan Sh100,000 mnamo Septemba 11 2017 ndipo asitekeleze agizo la kuwatimua katika jengo walimokuwa wakifanya biashara yao.

Bw Malunda alikabiliwa na shtaka la pili la kupokea hongo ya Sh30,000 kutoka kwa Bi Mandeep Channan kusudi asitekeleze agizo la kuwafukuza kutoka jengo walimokuwa wakifanyia biashara.

Mshtakiwa alimsihi Bw Kombo amwachilie kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu akisema , “ mshahara wangu ni Sh10,000 tu. Sina namna nyingine naweza kupata dhamana ya juu.”

Mshtakiwa alieleza korti kwamba tangu 2017 amekuwa akipiga ripoti kwa Kamishna wa kaunti ya Nairobi hadi jana alipoagizwa afike kortini kujibu shtaka.

“Nimekuwa mtu wa maadili mema. Nimekuwa nikiripoti kwa kamishna wa kaunti kila wiki hadi leo (jana) nilipoamriwa nifike kortini kujibu shtaka,” alisema Bw Malunda.

Pia mshtakiwa alimkabidhi hakimu nakala ya utaratibu jinsi amekuwa akiripoti kwa polisi na pia kwa afisi ya kamishna wa kaunti.

Lakini kiongozi wa mashtaka Bw Githinji Ndung’u aliomba korti itilie maanani makali ya adhabu atakayopata akipatikana na hatia na kuomba masharti ya dhamana yawe makali.

Hakimu alisema dhamana ni haki ya kila mshtakiwa na kumwachilia kwa dhamana ya Sh1.5milioni na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho.

Akishindwa kupata dhamana hiyo hakimu alimpa dhamana ya pesa tasilimu Sh100,000.

Watu wa familia ya mshtakiwa alifanya mchango kupata pesa za kumlipia dhamana hiyo ya pesa tasilimu.

Mahakama iliamuru kesi hiyo itajwe Januari 18 2021 kutengewa siku ya kusikizwa.

You can share this post!

Afiza wa zamani wa KDF asema polisi walitaka kumtia adabu

Chama cha ‘wilbaro’ chapata mwanga wa kusajiliwa