Habari Mseto

Chifu auawa na kuchomwa mazishini kwenye ghasia

December 17th, 2018 2 min read

IRENE MWENDWA Na GEORGE SAYAGIE

?Chifu mmoja katika Kaunti ya Marsabit aliuawa Jumapili na kisha mwili wake kuchomwa akihudhuria mazishi ya waathiriwa wa ghasia za kikabila ambazo zimeongezeka eneo hilo.

Naibu kamishna wa Kaunti Ndogo ya Saku, Bw Joseph Nyakwara alisema Chifu Biqa Godana wa lokesheni ya Qubi Kalo, aliuawa na mwili wake ukachomwa jana asubuhi.

Bw Nyakwara alisema chifu huyo alikuwa akihudhuria mazishi ya mmoja kati ya watu wawili waliouawa Jumamosi katika mzozo wa maji alipovamiwa, akauawa na kisha mwili wake ukachomwa.

Watu hao waliuawa pale jamii mbili zilipopigana eneo la Giresa. Bw Nyakwara aliambia Taifa Leo kwamba mtu mwingine amelazwa katika hospitali ya rufaa ya Marsabit akiwa na majeraha. Aliwataka wakazi kuacha tofauti zao na kudumisha amani.

Katika Kaunti ya Narok, serikali ililazimika kutangaza amri ya kutotoka nje kufuatia ghasia zilizozuka upya maeneo ya Ololoipangi, Nkoben Osananguriri na Oloruasi.

Kamishna wa kaunti hiyo George Natembeya, jana aliongoza kamati tya usalama kutembelea maeneo hayo na kutangaza amri hiyo kama njia moja ya kudumisha usalama katika eneo hilo linalokabiliwa na ghasia za kikabila.

“Ninataka kuwahimiza mkae ndani ya nyumba zenu kati ya saa kumi na mbili jioni na saa kumi na mbili asubuhi. Hakuna anayefaa kuwa nje katika masaa hayo,” alisema Bw Natembeya.

Kamishna huyo alifichua kuwa maafisa wa kikosi cha kupambana na fujo (GSU) wametumwa maeneo husika kutuliza hali.

“Tumetuma maafisa wa kuzima ghasia na wale wa GSU kwa sababu inaonekana ghasia hizo zinaongezeka. Tunataka kukabiliana na wanaopanga ghasia hizo,” alisema Bw Natembeya.

Mtu mmoja ameuawa na wengine 15 kujeruhiwa kwa mishale, ghasia zilipozuka upya katika maeneo ya Narok Kusini. Waliojeruhiwa wamelazwa katika hospitali tofauti eneo hilo.

Bw Natembeya alionya kuwa watakaokiuka kafyu hiyo watakamatwa. Kulingana na afisa huyo, uhasama kati ya Wamaasai na Wakipisigis ulianza Ijumaa na inaaminika ulitokana na wizi wa mifugo.

“Ni shambulio la kulipiza kisasi baada ya ng’ombe mmoja kushukiwa kuibwa eneo la Ololoipang’i na wezi kutoka jamii nyingine na kukasirisha wakazi wa vijiji vya Oloruasi na Nkoben.

Polisi walisema mtu aliyeuawa alijipata katikati ya ghasia hizo.