Habari Mseto

Chifu awekwa ndani kwa kukosa kuelezea bayana jinsi mwanamke alikufa

January 31st, 2024 1 min read

 NA GEORGE ODIWUOR

WATU watano akiwemo chifu wanahojiwa na polisi kuhusiana na kisa ambapo mwanamke mwenye umri wa miaka 60 alifariki katika nyumba yake huko Rangwe, Kaunti ya Homa Bay.

Chifu huyo ambaye aliteuliwa hivi majuzi alikamatwa na maafisa wa upelelezi kutoka kituo cha polisi cha Homa Bay, baada ya kudaiwa kukosa kuwapa maafisa wa usalama maelezo sahihi ya tukio la kifo katika eneo lake.

Alikamatwa pamoja na wanaume wengine wanne waliopeleka mwili wa marehemu mochari.

Wakazi waliripoti kuwa chifu alitoa idhini mwili wa mwanamke huyo uondolewe kutoka kwa nyumba yake hadi mochari.

Kulingana na Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Homa Bay Samson Kinne, wanaume hao watano ambao wanatoka eneo moja huko Rangwe walipeleka mwili wa marehemu mochari ya kibinafsi kwa kutumia gari la kibinafsi.

Hii ilikuwa baada ya mwanamke huyo kufariki katika hali isiyoeleweka.

Bw Kinne alisema chifu na wenzake waliripoti kwamba kulikuwa na kifo cha ghafla katika nyumba ya mwanamke huyo, wakilenga kumaanisha kuwa kifo chake kilikuwa cha kawaida kutokana na sababu za kiasili.

Zaidi ya hayo, ripoti hiyo ilitolewa baada ya mwili kuondolewa eneo la mauti.

Sheria inasema kisa kama hicho kinafaa kuripotiwa kwa polisi ili wafanye uchunguzi.