Habari Mseto

Chiloba kuitwa bungeni kujibu maswali licha ya kupigwa kalamu

October 24th, 2018 2 min read

Na CHARLES WASONGA

AFISA Mkuu mtendaji wa Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) aliyefutwa kazi, Ezra Chiloba, huenda akaitwa kufika mbele ya wabunge kujibu maswali kuhusu madai ya wizi au ubadhirifu wa Sh9.5 bilioni katika tume hiyo mwaka 2017. 

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu (PAC) Opiyo Wandayi (pichani) Jumatano alisema kuwa kamati yake itaanza uchunguzi kuhusu sakara hiyo Jumanne wiki ijayo.

“Tumewaita maafisa wote wote wa IEBC wakiongozwa na mwenyekiti wao Wafula Chebukati kuelezea jinsi pesa hizo zilitoweka au kuibiwa wakati wa uchaguzi mkuu uliopita, kama ilivyoelezwa kwenye ripoti ya Mhasibu Mkuu wa Serikali ya mwaka wa kifedha wa 2016/2017,” akasema Bw Wandayi.

“Wakati wa uchunguzi wetu, tutahitaji kupokea ushahidi kutoka kwa maafisa wengine ambao walikuwepo afisini wakati huo na wamejiuzulu au kufutwa kazi. Haswa tutahitaji kupata maelezo ushahidi kutoka kwa aliyekuwa afisa mkuu mtendaji Bw Ezra Chiloba ambaye alifutwa kazi juzi,” akaongeza mbunge huyo wa Ugunja.

Bw Wandayi alisema kuwa kamati yake imeamua kuharakisha uchambuzi kuhusu matumizi ya fedha katika IEBC mwaka ujao kwa sababu tume hiyo inakabiliwa na kibarua kigumu cha kuainisha upya mipaka na “kuandaa kura ya maamuzi” mwaka ujao.

“Tungetaka maswali yote kuhusu matumizi ya fedha katika IEBC mnamo mwaka wa kifedha wa 2016/2017 yapate majibu kabla ya mwaka ujao itakapaohitajika kuendesha shughuli ya mabadiliko ya mipaka. Pia itahitajika kuandaa kura ya maamuzi endapo mwafaka utapatikana kuhusu marekebisho ya katiba,” akaeleza Mbunge huyo wa Ugunja.

Kamati ya PAC imechukua hatua hii baada ya ripoti ya Mhasibu Mkuu wa Serikali Edward Ouko kudai kuwa takriban Sh9.5 bilioni hazijulikana ziilivyotumiwa wakati wa ununuzi wa vifaa vya uchaguzi vilivyotumika katika uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017.

Kulingana na ripoti hiyo, iliyowasilishwa bungeni wiki jana ununuzi wa bidhaa zilizotumika katika marudio ya uchaguzi wa urais Oktoba 26 pia ulikumbwa na hitalafu.

Mapema mwezi huu, Bw Chiloba, alifutwa kazi kutokana na madai kuwa alidinda kufika mbele ya kamati ya nidhamu ya IEBC kujibu masuala kuhusu madai ya matumizi mabaya ya pesa za umma wakati wa ununuzi wa vifaa vya uchaguzi mwaka jana.

Hii ni baada ya ripoti ya ukaguzi uliamriwa na IEBC mapema mwaka huu kubaini kuwa takriban Sh4.6 bilioni hzikutumika kwa mujibu wa sheria. Lawama zilionekana kuelekezwa kwa Bw Chiloba na ndio maana aliitwa kufika mbele ya kamati ya nidhamu kusudi ajitetee.

Bw Chebukati aliwaalika maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na wenzao wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuchunguza sakati hiyo kwa lengo la kuwachukulia hatua wahusika wote.

Hata hivyo, jana Bw Wandayi alisema uchunguzi wa kamati yake utaendeshwa kwa kuzingatia ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali wala sio ule ambao uliendeshwa na IEBC.