Habari Mseto

Chiloba sasa ataka Chebukati asukumwe jela kwa kumpiga kalamu

June 22nd, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

Afisa mkuu Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Bw  Ezra Chiloba aliwasilisha kesi tena mahakamani akipinga kusimamishwa kazi kwake.

Katika kesi hiyo Bw Chiloba anaomba mahakama imsukume jela mwenyekiti wa IEBC Bw Wafula Chebukati na makamishna wawili kwa kukaidi agizo wamrudishe kazini.

Bw Chiloba amewashtaki Mabw Chebukati na Makamishna Abdi Yakub Guliye na Boya Molu.

Bw Chiloba aliyewasilisha kesi hiyo chini ya sheria za dharura alisema maagizo yaliyotolewa wiki iliyopita iliuupuzwa na Mabw Chebukati, Guliye na Molu.

Wakili Andrew Wandabwa anayemwakilisha Bw Chiloba amesema kuwa maagizo ya mahakama arudishwe kazini yamepuuzwa.

Mahakama ya kuamua mizozo baina ya wafanyakazi na waajiriwa (ELRC) iliamuru Bw Chiloba arudishwe kazini huku ukaguzi wa ununuzi wa vifaa vilivyotumika wakati wa uchaguzi ukiendelea.

Siku hiyo IEBC iliamriwa imrudishe kazini Bw Chiloba alimwandikia barua aendelee kukaa nyumbani.

“Huku wakidharau maagizo ya hii korti washtakiwa walimwandikia barua nyingine ya kumsimamisha kazini Bw Chiloba,”  alisema Bw Wandabwa katika ushahidi aliowasilisha kortini.

Bw Wandabwa alisema hatua hii ni madharau ya hali ya juu na ukiukaji wa vipengee vya katiba.

Wakili huyo anaomba kesi hiyo isikizwe upesi kwa vile haki za Bw Chiloba zimekandamizwa na heshima kwa mahakama imeendelea kutiwa ndoa.

Jaji Onesmus Makau aliamuru mnamo Juni 14, aliamuru washtakiwa wamrudishe Bw Chiloba kazini.

Mnamo Oktoba 2017 Bw Chiloba alichukua likizo ya wiki tatu miito ajiuzulu ilipozidi. Wakati huo kampeini za uchaguzi wa kiti cha urais ulikuwa umepamba moto baada ya Mahakama ya Juu kuharamisha ushindi wa Rais Kenyatta.

Viongozi wa upinzani walikuwa wamechacha wakimtaka Bw Chiloba ajiuzulu baada ya Mahakama ya Juu kufutilia mbali ushindi wa Rais Kenyatta.

Bw Chiloba anaomba mahakama ibatilishe uamuzi wa kusimishwa kazi kwa mara ya pili.