Kimataifa

China bara kwa mara ya kwanza yakosa kisa chochote kipya cha maambukizi ya 'nyumbani' ya Covid-19

March 19th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

BEIJING, CHINA

KATIKA kile kinachoonekana ni mwanga wa mafanikio, China kwa mara ya kwanza katika kipindi cha majuma manane imekosa kisa chochote kipya cha maambukizi ya Covid-19 mkoani Hubei – kitovu cha janga hili – na China bara kwa jumla.

Hata hivyo, Tume ya Kitaifa ya Afya nchini humo imetoa takwimu zikionyesha kumekuwa na visa 34 vya maambukizi kutoka nje hasa miongoni mwa wasafiri wa kutoka ng’ambo, kwa mujibu wa data zilizotolewa Alhamisi.

Kumekuwa na vifo vipya vya wagonjwa wanane, vyote vikitokea mkoani Hubei.

Kufikia sasa China imehesabu maambukizi 189 ya kutoka nje, kumaanisha waathirika ni watu waliokuwa wamesafiri ng’ambo, na wala sio maambukizi ya nyumbani China.

Hali ya kawaida imeanza kurejea huku viwanda na biashara nyinginezo zikifunguliwa.

Takriban watu 80,928 wameugua Covid-19 nchini China ambapo 3,245 wamefariki huku 70,420 wakiwa wamepona kufikia sasa, kwa mujibu wa tume hiyo ya afya.

Virusi vipya hatari ambavyo vinasababisha Covid-19 viligunduliwa kwa mara ya kwanza Desemba 2019 mjini Wuhan, katikati mwa China.

Duniani kote kufikia sasa watu zaidi ya 200,000 wamepata maambukizi ambapo miongoni mwao 8,000 wamefariki kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO).