Kimataifa

China inavyotumia bata kukabili uharibifu wa nzige

February 24th, 2020 1 min read

MASHIRIKA na CHARLES WASONGA

SERIKALI ya China imewapeleka bata kwenye mipaka yake tayari kukabiliana na uvamizi wa nzige.

Ndege hao wamepelekwa katika eneo la mpaka la Xinjiang ambako China hupakana na Pakistan na India.

Katika vedeo iliyopeperushwa kupitia running ya kitaifa nchini China, CGTN ndege hao walionekana wakitembea wakielekea eneo la Xinjiang. Wanasayansi nchini China wanasema bata hao wanaweza kuwala nzige na hivyo kuzuia athari zake kwa mimea.

Nzige hao ambao wamavamia mataifa kadhaa katika ukanda kwa Afrika Mashariki kama vile Kenya, Uganda na Somalia, tayari wamevamia maeneo kadha ya India na Pakistan. Mataifa hayo ya bara Asia sasa yanakabiliwa na baa la njaa kwa sababu wadudu hao wameharibu mimea ya mashambani.

Serikali ya Pakistan, chini ya uongozi wa Waziri Mkuu Imran Khan, imetangaza uvamizi huo wa nzige katika hatari wa taifa kwa ni “uvamizi mbaya zaidi katika kipindi cha miongo kadha.”

Kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa, nzige husafiri kwa umbali ya wa hadi kilomita 200 kwa siku na wanaweza kula mimea yenye uzani sawa na ule wa miili yao kwa siku, Hii ina maana kuwa kundi dogo la nzige linaweza kula chakula ambacho kinaweza kutosha watu 35,000 kwa siku moja.

Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Chakula (FAO) limeonya kuwa ngize wanaweza kuathiri mataifa mengi na Afrika Mashariki na hivyo kuhatarisha maisha ya watu wengi.

Nzige hao ambao walionekana kwa mara ya kwanza mwezi Desemba mwaka tayari wameharibu maelfu ya ekari ya mashamba katika mataifa ya Kenya, Ethiopia, Somalia na Sudan Kusini. Watalaamu wanasema huu ndio uvamizi mbaya zaidi wa wadudu hao kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 70 iliyopita.