Kimataifa

China kuharibu pesa zote kuzima maambukizi zaidi

February 17th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

BENKI Kuu ya China imetangaza kuwa itaharibu pesa zote ambazo zimekusanywa na hospitali, mabasi na hata masoko katika maeneo ambapo virusi hatari vya Corona vimeshuhudiwa, kama njia moja wa kuzuia ueneaji wa virusi hivyo.

Mnamo Jumamosi, Benki Kuu iliagiza benki zote kuweka kando pesa zote zilizokusanywa katika maeneo ambapo virusi hivi vimesambaa, kuzisafisha halafu wazikabidhi benki hiyo.

Hii ni baada ya idadi ya watu ambao wameambukizwa homa hiyo kufika 70, 000 na walioaga dunia ni 1,670 kufikia Jumapili.

“Matrilioni ya pesa zimewekwa katika Benki Kuu kuanzia Januari 17 na kuna zile zilitoka katika eneo la Wuhan ambapo virusi hivi vilizuka,” alisema Fan Yifei, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya China.

Benki hiyo ilisema kuwa itatumia miale ya mwangaza wa Ultra-Violet (UV) na viwango vya juu vya joto ili kuua virusi hivyo vya Corona katika pesa hizo.

Pesa hizo zitawekwa kando kwa siku 14 kabla ya kuanza kusambazwa tena.

Hata hivyo, Yifei alisema kuwa Benki Kuu itaongeza fedha katika mabenki ili kusaidia biashara zisizorote katika msimu huu ambapo nchi hiyo inapambana na janga hili na vita vya kibiashara kati ya Amerika na China.

“Wateja wataulizwa ni wapi walitoa pesa zao lakini hatuna uhakika kuwa hatua hii itasaidia katika vita dhidi ya virusi hivi,” akasema naibu msimamizi wa benki moja.

Kulingana na wataalamu wa masuala ya uchumi, virusi vya Corona vitaathiri uchumi wa China na mataifa jirani ambapo sekta ya utalii na biashara za kusafirisha vitu ng’ambo zimeanza kuathirika katika nchi za Taiwan, Korea na Thailand.

Kwingine, polisi wa Hong Kong wanaendelea kuwatafuta wezi walioiba karatasi za chooni zenye thamani ya Sh13, 000 kutoka kwa duka moja, jana.

“Dereva wa lori moja alisimamishwa na wanaume watatu waliokuwa na visu nje ya duka moja katika eneo la Mong Kok na wakaiba karatasi hizo za chooni,” akasema msemaji wa polisi.

Karatasi za chooni zimekuwa miongoni mwa bidhaa ambazo zimeadimika sana katika eneo hilo hata baada ya serikali kuwahakikishia kuwa bidhaa za matumizi ya kila siku zitaendelea kusambazwa kama kawaida.

Pia bidhaa kama mchele na spaghetti ambazo ni vyakula vinavyoliwa sana na Wachina vimepungua.