Kimataifa

China yadai virusi vya corona vilisambazwa na jeshi la USA

March 14th, 2020 2 min read

Na AFP

AFISA wa cheo cha juu wa China amedai huenda jeshi la Amerika lilipeleka virusi hatari vya corona nchini humo huku maradhi hayo yakiendelea kuenea mataifa mbalimbali na kuua watu zaidi ya 5,000.

Bila kufafanua, msemaji wa wizara ya ulinzi wa China, Zhao Lijian, aliandika kwenye Twitter kwamba, kuna uwezekano virusi hivyo vilipelekwa China na wanajeshi wa Amerika.

Dai lake linawiana na habari zilizoenezwa kwenye mitandao ya kijamii nchini China zikilaumu Amerika kwa mkurupuko huo.

Mkuu wa kituo cha kudhibiti maradhi nchini China amesema, maradhi hayo yalianza soko la Wanyama katika jiji la Wuhan.

Hata hivyo, maafisa wa China na wataalamu mashuhuri wa afya wanadai huenda virusi hivyo vilitoka kwingineko. China imefokea maafisa wa Amerika wanaoita maradhi hayo “virusi vya Wuhan.”

Kwenye ujumbe wake wa Twitter, Zhao alipakia video ya mkuu wa kituo cha kuzuia maradhi cha Amerika akiwa mbele ya bunge la Congress akisema, baadhi ya raia wa Amerika ambao waliaminika kuuawa na homa baadaye iligunduliwa walikuwa na virusi vya corona.

“Inawezekana jeshi la Amerika lilileta maradhi haya Wuhan. Semeni ukweli! Fichulieni umma habari mlizonazo. Amerika inafaa kutueleza ukweli,” alisema Zhao Ijumaa na kuambatisha makala aliyosema yalikuwa ushahidi kwamba virusi hivyo vilianzia Amerika.

Maafisa wa China wamelaumiwa kwa kujaribu kuficha virusi hivyo huku polisi jijini Wuhan wakitisha madaktari waliozifichua Desemba mwaka jana.

Maafisa wa Amerika wamelaumu China kwa kuhusisha nchi yao na virusi hivyo huku waziri wa Mashauri ya Kigeni Mike Pompeo akiviita virusi vya Wuhan.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya China imekataa jina hilo na kulitaja kama kukosea heshima sayansi. Watu zaidi ya 130,000 wameambukizwa virusi hivyo na 5000 wamekufa kote ulimwenguni.

Mshauri wa masuala ya usalama wa Amerika Robert O’Brien, amesisitiza kuwa maradhi hayo yalianzia China.

“Virusi hivi havikuanzia Amerika, vilianzia Wuhan,” O’Brien alisema. “Hata hivyo, inasikitisha, badala ya kuchukua hatua zinazofaa, mkurupuko huu ulifichwa,” alisema. Alisema China ilifanya ulimwengu kuchukua miezi miwili kabla ya kujipanga kukabili maradhi hayo.

“Kama China ingeshirikiana na kuruhusu wataalamu wa kigeni kufika yalikoanzia, tungekuwa tumezuia kilichotokea China na sasa kinafanyika kote ulimwenguni,” aliongeza Obrien.

Mnamo Alhamisi mke wa waziri mkuu wa Canada Justin Truadeau alipatikana kuwa na homa hiyo baada ya kuzuru Ulaya na kufanya ajitenge.