Habari Mseto

China yaipa Kenya msaada wa mchele magunia 90,000

February 19th, 2018 1 min read

Na WINNIE ATIENO

SERIKALI ya Uchina imeipa Kenya msaada wa mchele ili kukabiliana na baa la njaa linaloendelea kukumba sehemu mbalimbali humu nchini.

Akipokea msaada huo wa magunia 90,000 ya mchele katika bandari ya Mombasa, Jumamosi, Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa alisema chakula hicho kitatolewa kwa wakazi wanaokumbwa na baa la njaa kukabiliana na janga hilo.

Aidha, Bw Wamalwa alisema serikali imeweka mikakati kabambe ya kukabiliana na njaa ikiwemo kuimarisha kilimo cha unyunyiziaji mimea maji.

Aliilaumu kiangazi kusababisha njaa hususan katika kaunti za maeneo kame kama Wajir, Mandera, Garissa na Isiolo.

“Maafisa husika wafanye bidii ili chakula hiki kiwafikie wahanga wa njaa. Wakenya msiwe na wsiwasi msaada umefika, sasa kuna chakula.

Mchele huu utapelekwa Isiolo ambapo kuna hatari ya njaa, vile vile Wajir, Garissa, Mandera miongoni mwa sehemu nyingine humu nchini,” akasema waziri huyo.  Alisema kuna uhaba mkubwa wa mchele humu nchini.

“Tuna mahindi, maharagwe na mafuta ya kupikia; kilichobakia ni mchele ambao tunaagiza sababu ya uhaba.  Ni majuzi tu ambapo tulizindua ujenzi wa bwawa la Thiba huko Kirinyaga ambalo litaongeza zao la mchele katika mradi wa umwagiliaji maji wa Mwea,” Bw Wamalwa akasema.

Ujenzi huo utakapomalizwa, Bw Wamalwa alisema utazalisha mchele wa tani 80,000 hadi 160,000 kwa mwaka. Ujenzi huo utagharimu Sh20 bilioni. Kwa sasa mradi huo unazalisha tani 80,000 za mchele.

“Tutaimarisha miradi kadhaa ya umwagiliaji maji eneo la Nzoia ambayo pia itaongeza mazao, ile ya Soin-Koru miongoni mwa mingine,” akasema Bw Wamalwa. Katika eneo la Pwani, Kaunti ya Tana River inakabiliwa na ukosefu wa mazao kutokana na kiangazi.

Gavana Dhadho Godhana atanunua tani 40 ya mahindi kwa wakulima wa Bura ili kusambaza kwa wakazi wanaokabiliwa na baa la njaa kutokana na kiangazi.