Habari Mseto

China yatetea idadi kubwa ya kampuni zake nchini Kenya

March 20th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

CHINA imejitetea kuhusu hali ya kampuni zake kumiminika humu nchini, ikisema zinakuja kutafuta watu wa kuajiri kwa kuwa hakuna vijana wa kutosha nchi hiyo.

Maafisa wa serikali ya China aidha wamesema kuwa upungufu wa ardhi kwao ndio unafanya nyingi za kampuni zake kuhamishia shughuli barani Afrika, kwa kuwa mazingira ya kazi nyumbani kwao yameharibika.

Madai haya yalitolewa jana wakati maafisa hao walifanya kikao na wenzao wa Kenya, kujadili masuala kadhaa, yakiwemo wingi wa kampuni hizo nchini na hali ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).

“Kampuni za China zinajipa moyo kuhamia barani Afrika kutokana na sheria ya kila wanandoa kuzaa mtoto mmoja pekee ambayo iliwekwa miaka ya nyuma. Kwa sasa, kizazi cha vijana nyumbani kina watu wachache sana ikilinganishwa na wakati wetu ambapo kulikuwa na wafanyakazi wa kutosha,” akasema afisa kutoka China.

Aliongeza, “Kampuni nchini China zinakumbana na matatizo kutafuta wafanyakazi na kulipa mshahara wa juu. Hii ni licha ya kuwa ardhi pia imekuwa ndogo kufanya maendeleo. Hivyo, kampuni nyingi zinakuja kuwekeza Afrika na kutafuta nafasi za biashara, huku zikihamishia viwanda huku.”

Afisa huyo alisema hayo akiwarai viongozi na Wakenya kupokea kampuni hizo zinapokuja, akiongeza kuwa mnamo Desemba na Novemba pekee mwaka jana, zaidi ya kampuni 200 za kutoka China ziliwasili nchini kutafuta fursa za uwekezaji.

Katika kikao hicho, suala la hali ya ujenzi wa reli ya SGR aidha liliangaziwa, ambapo maafisa hao wa China waliteta kuhusu mjadala ambao umekuwa ukiendelea miongoni mwa Wakenya, wengi wakikashifu kampuni za China, hasa zinazohusika na ujenzi wa SGR.

China vilevile, ilisema iko tayari kuunga mkono Kenya kuwania kiti katika baraza la Usala la Umoja wa Mataifa, endapo tu itaruhusiwa na Muungano wa Afrika (AU).