Na JOHN KIMWERE
Ni kati ya wanamaigizo wa kike wanaopania kufanya makubwa katika tasnia ya burudani miaka ijayo. Bila kuongeza chumvi wala kupaka mafuta kwenye mgongo wa chupa sekta ya uigizaji hapa nchini inazidi kuimarika.
Hildah Muhonja Murichoh maarufu Chinese ni miongoni mwa wasanii wanaopiga dili mbali mbali kwenye juhudi za kusaka posho. Kipusa huyu aliyezaliwa mwaka 1994 pia ni mpondoaji (Makeup Artist) bila kuweka katika kaburi la sahau meneja wa baadhi ya wasanii wanaoibukia.
”Bila kusahau nakumbuka nilianza kuvutiwa na masuala ya uigizaji tangu nilipojiunga na Shule ya Upili ya Butere Girls,” anasema na kuongeza kuwa ni uamuzi aliofikia baada ya kutazama filamu iitwayo ‘Selina’ walioshiriki Celestine Gichuhi na Natasha Sanaipei Tande kati ya wengine. Kwa jumla kisura huyu anajivunia kushiriki filamu kadhaa ikiwamo ‘Auntie Boss,’ Andakava,’ ‘Varshita,’ ‘Selina,’ ‘Hullabaloo,’ na ‘Zora’ inayozidi kuchota wapenzi wa maigizo kupitia Citizen TV.
Viola Davis
”Sina shaka kutaja kuwa kila msanii hupania kutinga hadhi ya juu kisanaa. Binafsi ninalenga makubwa katika masuala ya uigizaji ambapo ninalenga kufuata nyayo za kati ya waigizaji wa kimataifa kama Viola Davis mzawa wa Marekani,” asema na kuongeza kuwa ndani ya miaka mitano ijayo anataka kufungua taasisi ya kufunza masuala ya uigizaji pia urembo.
Anapenda kushirikiana nao Sarah Hassan ambaye hushiriki naye kwenye kipindi cha Zora (Citizen TV). Pia anasema kuwa anatamani sana kufanya kazi na Natasha Sanaipei Tande ambaye pia alishiriki filamu ya Plan B. Anasema kuwa kimataifa angependa kufanya kazi na wana maigizo mahiri kama Omotola Jalade Ekeinde na Abimbola Aisha Ademoye maarufu Bimbo wote wazawa wa Nigeria.
Wakili
Ingawa dada huyu amekumbatia masuala ya burudani anadokeza kuwa tangia akiwa mtoto alitamani sana kuhitimu kuwa wakili. Anasema kuwa kinyume na miaka iliyopita wengi wametambua uigizaji ni ajira kama zingine lakini tatizo lililopo ni kuwa hapa nchini malipo ni duni. Anapendekeza serikali ipunguze ada ya kupata idhini kuchukua filamu mijini maana hali hiyo imezuia wasanii wa kigeni kufanyia shughuli zao hapa nchini.
Anadokeza kuwa anadhani Wakenya wengi hupenda kutazama filamu za kigeni maana kazi za wazalendo hukosa mvuto. Akijibu swali kama ana mpenzi alidokeza kuwa team mafisi wamsahau maana tayari ana sabuni ya roho wanaopania kuanzisha familia naye miaka ijayo. Hata hivyo anakiri kuwa ni kawaida kwa warembo kutongozwa lakini lazima kila mmoja ana msimamo wake.
Ushauri
Anashauri wenzie kuwa wasiwe wanatarajia makubwa wanapojiunga na uigizaji. ”Ninaamini ni muhimu sana wasanii tuwe tunasaidiana kwa masuala mbali mbali tuache kukomoana. Wenzetu wengine hasa waliotutangulia wameibuka kivingine ambapo huwa hawapendi kutambua wasanii chipukizi,” akasema. Kadhalika anashauri kuwa wawe wabunifu pia kamwe wasivunjike moyo.