Michezo

Chipu kusaka muujiza dhidi ya Japan Raga ya Dunia U-20

July 17th, 2019 3 min read

Na GEOFFREY ANENE

MAKOCHA Paul Odera (Kenya) na Yoshitake Mizuma (Japan) wametaja vikosi vyao kabla ya mechi ya Raga ya Dunia ya wachezaji 15 kila upande ya chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 itakayosakatwa uwanjani Martins Pereira mjini Sao Paulo nchini Brazil mnamo Jumatano saa tano usiku.

Odera amefanya badiliko moja pekee katika kikosi chake ambacho kimepata kupumua baada ya nyota Andrew Siminyu, Jeff Mutuku na Douglas Kahuri kuondolewa katika orodha ya majeruhi.

Siminyu, ambaye ni mwanafunzi nchini Afrika Kusini, ataanza mchuano huu wa mwisho wa Kundi B, huku wachezaji wa klabu ya Kenya Harlequin Mutuku na Kahuri wakitiwa kwenye benchi.

Siminyu aliumia kifundo dhidi ya Brazil mnamo Julai 13. Mutuku na Kahuri walijeruhiwa kifundo na mguu mtawalia katika mechi ya ufunguzi dhidi ya Uruguay mnamo Julai 9.

“Ni kweli, wachezaji hao (Siminyu, Mutuku na Kahuri) wamepona. Michelle Brighetti aliumia mazoezini. Yeye pekee ndiye atakosa mchuano huu,” Odera aliambia Taifa Leo baada ya kutaja kikosi kitakachoanza dhidi ya mabingwa wa mwaka 2014 na 2017 Japan.

Barry Robinson kutoka klabu ya Kabras Sugar ndiye badiliko pekee lililofanywa na Odera katika kikosi cha wachezaji 15 wa kwanza. Robinson anajaza nafasi ya Brighetti kati ya uwanja (nafasi ya 9). Nahodha msaidizi Samuel Asati ataanza kutoka kitini.

Kuhusu kibarua kinachosubiri Chipu, Odera alisema, “Tunakutana na timu inayoorodheshwa nambari moja katika mashindano haya kwa hivyo, ni mechi ngumu kabisa tutacheza hapa. Vijana wamejawa na matumaini, lakini pia wana tumbo joto.”

Nahodha Boniface Ochieng’ na nahodha msaidizi Dominic Coulson walikubaliana na maoni ya Odera kuwa Japan ni timu kali.

“Tunacheza dhidi ya mojawapo ya timu zilizo na uzoefu wa miaka mingi na iliyo na nidhamu ya hali ya juu katika mashindano haya. Huu ndio mtihani wetu mkali zaidi na ambao utatupatia picha kamili umbali tumefika katika timu ya taifa. Nafurahia mtazamo wa wachezaji wenzangu na jinsi mambo yalivyo, tutajitahidi kadri ya uwezo wetu kuonyesha uwezo wetu,” Ochieng’ aliambia Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) katika mahojiano mengine.

Coulson, ambaye alipachika kiki la alama tatu lililowezesha Kenya kuzamisha Brazil 26-24 Julai 13, alisema, “Bila shaka, itakuwa mechi yetu ngumu kabisa. Japan ni timu nzuri sana. Tumejitahidi kutambua makosa yao na katika mazoezi yetu juma hili, tumeangazia njia nzuri ya kutumia ulegevu wao kwa manufaa yetu.”

Japan imefanyia kikosi chake mabadiliko makubwa sana, ikianzisha wachezaji wengi waliokuwa kitini dhidi ya Uruguay na kuwatia walioanza mechi hiyo kwenye benchi.

Wajapani walipepeta Uruguay 46-31 na Brazil 56-24 katika mechi zao mbili za kwanza na wanapigiwa upatu kutesa mabingwa wa Afrika, Kenya, ambao watahitaji muujiza kupata ushindi ama sare.

Viongozi Japan wamezoa alama 10, pointi nne zaidi ya mabingwa wa mwaka 2008 Uruguay. Kenya na Brazil wanashikilia nafasi mbili za mwisho kwa alama nne na mbili, mtawalia. Chipu ilicharazwa 63-11 na Uruguay katika mechi yake ya ufunguzi Julai 9.

Ureno na Tonga wako sako kwa bako juu ya Kundi B kwa alama 10 kila mmoja. Watalimana katika mechi ya mwisho ya kuamua mshindi wa kundi hili. Canada imezoa alama mbili nayo Hong Kong iko mkiani bila alama.

Washindi wa makundi yote mawili watakabiliana katika fainali Julai 21 kuamua timu itakayopandishwa ngazi kushiriki Raga ya Dunia ya daraja ya juu kabisa (JWC) mwaka 2020 kuchukua nafasi ya Scotland iliyoshushwa kushiriki mashindano haya ya daraja ya pili (JWT).

VIKOSI

Kenya: Wachezaji 15 wa kwanza – 1. Andrew Siminyu, 2. Bonface Ochieng (nahodha), 3. Ian Masheti, 4. Emanuel Silungi, 5. Hibrahim Ayoo, 6. Samuel Were, 7. Brian Amaitsa, 8. George Kyriazi, 9. Barry Robinson, 10. Dominic Coulson, 11. Timothy Omela, 12. John Okoth, 13. James Mcgreevy, 14. Geofrey Okwach, 15. Andrew Matoka; Wachezaji wa akiba – 16. Wilfred Waswa, 17. Ian Njenga, 18. Rotuk Rahedi, 19. Collins Obure, 20. Frank Aduda, 21. Sheldon Kahi, 22. Samuel Asati, 23. Owain Ashley, 24. Jeff Mutuku, 25. Douglas Kahuri.

Japan: Wachezaji 15 wa kwanza – 1.Gun Tajima, 2.Daiki Nishiyama, 3.Shohei Tsujimura, 4.Koki Matsumoto, 5.Shu Yamamoto, 6.Akito Okui, 7.Hayato Fukunishi, 8.Shota Fukui (nahodha), 9.Ryota Tomoike, 10.Takumi Aoki, 11.Moeki Fukushi, 12.Taihei Kusaka, 13.Tomoki Osada, 14.Halatoa Vailea, 15.Keita Inayoshi; Wachezaji wa akiba – 16.Terutaka Oka, 17.Yota Kamimori, 18.Sho Maeda, 19.Mamoru Harada, 20.Takamasa Maruo, 21.Kaisei Tamura, 22.Ryuto Fukuyama, 23.Futo Yamaguchi, 24.Ryosuke Kawase