Michezo

Chipukizi 99 kung'ang'ania nafasi katika Harambee Stars U-20

February 15th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKISHO la Soka la Kenya (FKF) limealika wachezaji 99 kwa majaribio ya kuunda timu ya taifa ya Under-20 yatakayoanza Februari 19, 2018 uwanjani Kasarani, Nairobi.

Kikosi cha kwanza cha wachezaji 50 kitajaribiwa Februari 19 na Februari 20, huku kundi la pili likijaribiwa Februari 21 na Februari 22.

Taarifa kutoka FKF zimesema Jumatano kwamba wachezaji wa kimataifa na wale watakaotambuliwa kutoka kwa mashindano ya Chapa Dimba Na Safaricom ya mikoa ya Kati na Nairobi watajiunga na timu juma lijalo.

Wachezaji 99 walioitwa kwa majaribio walitambuliwa katika mashindano ya Chapa Dimba Na Safaricom, ambayo bado yanaendelea, na Ligi za FKF. Kocha Mkuu wa zamani wa timu ya taifa ya watu wazima, Harambee Stars, Stanley Okumbi aliongoza shughuli ya kutafuta talanta hiyo changa.

Timu ya taifa ya Under-20 ya wanaume, ambayo inajulikana kama Rising Stars, itapimana nguvu na Tanzania jijini Dar es Salaam mapema mwezi Machi kabla ya kuelekea nchini Misri kwa mashindano ya mwaliko ya mataifa manne yatakayofanyika jijini Cairo kutoka Machi 18 hadi Machi 28, 2018.

Kenya itatumia mechi hizo kujitayarisha kwa michuano ya kufuzu kushiriki mashindano ya Afrika ya Under-20, ambayo inatarajiwa kuandaliwa nchini Niger mwaka 2019.