Michezo

Chipukizi Leao wa AC Milan aweka rekodi ya kufunga bao la haraka zaidi katika historia ya Serie A

December 20th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

RAFAEL Leao, 21, alifunga bao la haraka zaidi katika historia ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) alipowaongoza waajiri wake AC Milan kutikisa nyavu za Sassuolo baada ya sekunde sita pekee mnamo Disemba 20, 2020.

AC Milan ambao kwa sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 31, waliipepeta Sassuolo 2-1 katika mechi hiyo ya Jumapili usiku.

Leao ambaye ni fowadi matata raia wa Ureno, alikamilisha kwa ustadi pasi aliyopokezwa na Hakan Calhanoglu na kuwapa AC Milan motisha ya kuendeleza rekodi ya kutopigwa hadi kufikia sasa kwenye kampeni za Serie A msimu huu.

Bao la Leao lilivunja rekodi ya Piacenzo Paolo Poggi aliyewahi kufungia AC Milan dhidi ya Fiorentina baada ya ya sekunde 8.9 za ufunguzi wa kipindi cha kwanza mnamo Disemba 2, 2001.

Goli la Leao lilikuwa la haraka zaidi kuliko hata linaloshikilia rekodi katika soka ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na ambalo lilifungwa na Shane Long wa Southampton dhidi ya Watford baada ya sekunde 7.69 pekee mnamo Aprili 23, 2019.

AC Milan kwa sasa wanadhibiti kilele cha jedwali la Serie A kwa alama moja zaidi kuliko nambari mbili Inter Milan waliowapokeza Spezia kichapo cha 2-1.

Kiungo raia wa Ubelgiji, Alexis Saelemaekers alifunga bao la pili la AC Milan katika dakika ya 26 kabla ya Domenico Berardi kufutia Sassuolo machozi mwishoni mwa kipindi cha pili.

Matokeo hayo yaliwasaza Sassuolo katika nafasi ya sita jedwalini kwa alama 23, moja nyuma ya nambari tano AS Roma waliopokezwa kichapo 4-1 na Atalanta.