Chipukizi Mason Greenwood sasa kuchezea Manchester United hadi 2025

Chipukizi Mason Greenwood sasa kuchezea Manchester United hadi 2025

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI chipukizi wa Manchester United, Mason Greenwood, 19, amerefusha mkataba wake uwanjani Old Trafford hadi Juni 2025 na atakuwa radhi kuongeza mwaka mwingine mmoja zaidi kufikia wakati huo.

Sogora huyo aliwajibishwa na Man-United kwa mara ya kwanza katika kikosi chao cha watu wazima mnamo Septemba 2020 na wakati huo alikuwa na kandarasi iliyotarajiwa kutamatika mnamo Juni 2023.

Greenwood alipokezwa malezi ya kusakata soka katika akademia ya Man-United na amekuwa na kikosi hicho tangu akiwa na umri wa miaka saba pekee.

Kufikia sasa msimu huu, amefungia waajiri wake mabao manne kutokana na mechi 18, ufanisi unaofikisha magoli yake hadi 21 kutokana na mechi 82 akiwa mchezaji wa Red Devils.

Kocha Ole Gunnar Solskjaer alimchezesha Greenwood kwa mara ya kwanza kambini mwa Man-United mnamo Machi 2019, mshambuliaji huyo akiwa na umri wa miaka 17 na siku 156.

Katika kampeni za msimu wa 2019-20, Greenwood alifungia Man-United jumla ya mabao 17 kutokana na mapambano yote na goli lake la hivi karibuni zaidi akichezea mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ni dhidi ya Liverpool kwenye Kombe la FA mnamo Januari 2021.

Chipukizi huyo aliwajibishwa na timu ya taifa ya Uingereza kwa mara ya kwanza kwenye mechi ya Uefa Nations League dhidi ya Iceland mnamo Septemba 2020 akiwa pamoja na kiungo Phil Foden wa Manchester City. Hata hivyo, walitemwa kambini mwishoni mwa mechi hiyo baada ya kukiuka kanuni za kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

TAFSIRI NA:CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Difenda David Alaba kuondoka Bayern Munich baada ya...

Atupwa jela miaka mitatu kwa kuiba chupi