Michezo

Chipukizi mzawa wa Ujerumani anayechezea Bayern Munich aitwa kambini mwa chipukizi wa timu ya taifa ya Uingereza

November 6th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

FOWADI wa Bayern Munich, Jamal Musiala na beki Lee Buchanan wa Derby County wameitwa kwa mara ya kwanza kambini wa timu ya taifa ya Uingereza ya chipukizi wasiozidi umri wa miaka 21.

Wawili hao ni sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na kocha Aidy Boothroyd katika mechi mbili zijazo dhidi ya Andorra mnamo Novemba 13 kisha Albania mnamo Novemba 17, 2020.

Uingereza watajitosa ugani kwa minajili ya mechi hizo wakijivunia tayari kufuzu kwa fainali za Euro 2021 kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 21.

“Ukweli kwamba tayari tumejikatia tiketi ya Euro zikisalia mechi mbili zaidi ni ishara kwamba tunajivunia kikosi bora kinachotawaliwa na kiu ya kutwaa mataji ya haiba,” akasema Boothroyd.

“Ina maana kwamba sasa tunaweza kuwapa wachezaji wengine jukwaa la kudhihirisha ukubwa wa uwezo wao uwanjani. Baadhi ya wanasoka hao ni Jamal Musiala na Buchanan,” akaongeza kocha huyo.

Buchanan alipokezwa malezi ya soka kambini mwa Derby County huku Musiala, 17, akiwa chipukizi wa zamani wa Chelsea.

Musiala alijiunga na Bayern mnamo 2019 na akawajibishwa na miamba hao wa Ujerumani mara 19. Mapema msimu huu wa 2020-21, alifunga bao lake la kwanza la Bundesliga na kuweka historia ya kuwa mchezaji mchanga zaidi kuwahi kufunga bao akivalia jezi za miamba hao wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Buchanan, 19, amechezea Derby County mara tisa pekee hadi kufikia sasa msimu huu wa 2020-21.

KIKOSI CHA UINGEREZA

MAKIPA: Brandon Austin (Tottenham), Josef Bursik (Stoke, on loan at Doncaster), Aaron Ramsdale (Sheffield United);

MABEKI: Max Aarons (Norwich), Lee Buchanan (Derby), Marc Guehi (Chelsea, kwa mkopo Swansea), James Justin (Leicester), Lloyd Kelly (AFC Bournemouth), Tariq Lamptey (Brighton), Jonathan Panzo (Dijon), Rhys Williams (Liverpool), Ben Wilmot (Watford);

VIUNGO: Jude Bellingham (Borussia Dortmund), Josh Dasilva (Brentford), Ebere Eze (Crystal Palace), Conor Gallagher (Chelsea, kwa mkopo West Bromwich Albion), Curtis Jones (Liverpool), Oliver Skipp (Tottenham, kwa mkopo Norwich);

WAVAMIZI: Rhian Brewster (Sheffield United), Callum Hudson-Odoi (Chelsea), Dwight McNeil (Burnley), Jamal Musiala (Bayern Munich), Eddie Nketiah (Arsenal), Ryan Sessegnon (Tottenham, kwa mkopo Hoffenheim).