Michezo

Chipukizi wa Isiolo Young Stars wanaopania makubwa

March 18th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya wavulana ya Isiolo Young Stars inalenga kunoa makucha yake kuhakikisha inaibuka kati ya vikosi mahiri kwenye soka ya eneo la Isiolo miaka ijayo.

Pia inalenga kukuza talanta za chipukizi wake angalau wakomae kiwango cha kuteuliwa kupigia timu za taifa kwa wasiozidi umri wa miaka 20.

Ingawa iliasisiwa mwaka uliyopita imeonyesha ustadi wake baada ya kuibuka ya pili kwenye mechi za Chapa Dimba na Safaricom Season Two katika Mkoa wa Mashariki katika fainali zilizochezewa Kitui Show Ground wiki iliyopita.

Isiolo Young Stars ya kocha, Martin Mutembei ilimaliza ya pili ilipozabwa mabao 5-4 na Super Solico ya Mwingi kupitia mikwaju ya penalti baada ya kutoka sare bao 1-1.

Kwenye nusu fainali, Isiolo Young Stars iliinyanyua Triumph kutoka Embu mabao 2-0 nayo Samba FC ya Marsabit ilichomwa mabao 3-2 na Super Solico.

”Chipukizi wangu walizoa tiketi ya kushiriki fainali za Mkoa baada ya kubeba ubingwa wa mechi hizo Tawi Ndogo la FKF Meru,” alisema kocha huyo na kuongeza kuwa haikuwa mteremko.

Kwenye michezo hiyo wavulana haoi walipiga Nkanda Boys mabao 2-0 kisha kutoka sare tasa dhidi ya Meru Talents. Kwenye mechi za mashinani Tawi la Isiolo, vijana hao walirarua Taqwa Youth kwa mabao 2-0 na kuvuna ushindi wa magoli 4-2 mbele ya Real Silver.

”Licha ya kutofuzu kwa fainali za kitaifa matokeo ya vijana wangu wameonyesha wamepania kufanya makubwa,” alisema mwenyekiti wake Mohammed ‘Kaka J’ Abdikarim na kuongeza kuwa ana imani kikosi hicho kitatawala soka ya eneo hilo.

Alidokeza kuwa eneo hilo limefurika chipukizi wengi wenye talanta za michezo mbali mbali lakini uhaba wa wadhamini umefanya nyingi kuyeyuka kwa kutotambuliwa. Isiolo Young Stars hufanyia mazoezi katika Uwanja wa Wabera mjini humo.

Kocha huyo anapongeza wachana nyavu hao kwa kazi nzuri waliofanya licha ya kutotimiza azimio la kusonga mbele. Fainali za kitaifa zitaandaliwa katika Kaunti ya Meru, Kinoru Stadium mjini humo.

”Bila shaka wachezaji wetu walionyesha mchezo safi kwenye kampeni hizo ambapo hatuna budi kuwapongeza,” alisema na kuongeza kuwa wataanza kushiriki mechi za kujimana nguvu na majirani zao kujiandalia michezo ijayo.

Alidokeza kwamba mwanzo wanalenga kushiriki mchezo wa kirafiki dhidi ya Sofapaka Youth kwa wasiozidi umri wa miaka 20 ya Nairobi. Kocha huyo alisema kando na kikosi hicho wanazo timu zingine (U12, U15 na U17).

Isiolo Young Stars inashirikisha chipukizi kama:Abdulmalik Enow, Mohamed Ali, Abubakar Ibrahim (nahodha), Abdisalan Ibrahim, Dennis Mureithi, Evans Mwiti, Mohamed Abdi, Mohamed Aliow, Joseph Kariuki, Abdiamin Issack, Ken Mutuma, Antanasio Echipi, Abdinasir Abdikadir, Farah Abdi na Denis Mureithi.

Wengine wakiwa Peter Maina, Frankline Mwenda, Abdirizack Rashid, Evans Muthuri, Sammy Njuguna, Silas Mbaabu na Daniel Mutembei.