Chipukizi wa Uingereza U-19 wazamisha Israel na kutwaa taji la Euro

Chipukizi wa Uingereza U-19 wazamisha Israel na kutwaa taji la Euro

Na MASHIRIKA

UINGEREZA walitoka nyuma kwa bao moja na kufunga mabao mawili katika muda wa ziada katika ushindi wa 3-1 waliousajili dhidi ya Israel kwenye fainali ya Euro kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 19.

Oscar Gloch aliwaweka Israel kifua mbele katika dakika ya 40 kabla ya Callum Doyle kusawazishia Uingereza kunako dakika ya 52. Mechi hiyo ilichezewa nchini Slovakia.

Carney Chukwuemeka wa Aston Villa alifunga bao la pili la Uingereza katika dakika ya 108 kabla ya Aaron Ramsey kupachika la tatu dakika nane baadaye.

Ni mara ya pili baada ya kipindi cha miaka mitano kwa Young Lions wa Uingereza kushinda kipute cha Euro U-19. Kipa wa sasa wa Arsenal, Aaron Ramsdale na kiungo Mason Mount wa Chelsea walikuwa sehemu ya kikosi kilichozolea Uingereza taji la Euro U-19 mnamo 2017.

Miongoni mwa wanasoka waliopongeza chipukizi wa Uingereza ni fowadi matata wa Tottenham Hotspur, Harry Kane aliyeandika kwenye mtandao wa kijamii: “Vijana werevu! Mmefanya kazi kubwa na nzuri. Furahieni ushindi wenu huo.”

Uingereza wanaonolewa na kocha Ian Forster waliongoza kampeni zao za makundi kabla ya kutoka nyuma na kukomoa Italia kwenye nusu-fainali. Israel kwa upande wao, waliingia fainali baada ya kuduwaza Ufaransa kwenye nusu-fainali.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Jumwa amsifia Ruto, asema ndiye suluhu ya uchumi wa nchi...

Sh143b kutumika kwa ujenzi wa miji 3 ya Lapsset

T L