Bambika

Chipukizi wanaopania kuleta mwamko mpya katika Injili nchini

February 18th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

KWA miaka kadhaa sasa, kumekuwa na pengo kubwa katika tasnia ya muziki wa Injili nchini.

Hili linafuatia hatua ya baadhi ya wanamuziki maarufu walioidhibiti tasnia hiyo kuhamia katika “miziki ya kidunia”, hivyo kuacha pengo kwenye utunzi wa nyimbo za injili.

Tangu 2010, baadhi ya wanamuziki waliosifika  kwa kuishikilia tasnia hiyo ni Willy Paul, Bahati, Hopekid, Mr Seed, Masterpiece, Gloria Muliro kati ya wengine.

Katika enzi zao, wanamuziki hao walisifika kote kote.

Wao ndio walikuwa washindani wakuu katika mashindano yoyote yale ya nyimbo za injili—kama vile Groove Awards na Mwafaka Awards.

Mashindano yoyote ya nyimbo za injili hayangeonekana ‘kukamilika’, hasa bila kujumuishwa kwa wasanii Willy Paul au Bahati, kwani waliibukia kuwa kama ‘wafalme’ katika tasnia hiyo.

Wafuatiliaji wa masuala ya burudani pia wamekuwa wakitaja kuondolewa kwa mashindano kama Groove Awards kama moja ya sababu zilizochangia wanamuziki wengi kuondoka katika tasnia hiyo.

Hata hivyo, baada ya wasanii hao kuondoka katika tasnia hiyo, kumechipuka kizazi kipya cha wanamuziki, wanaosema kuwa lengo lao ni kujaza pengo lililoachwa na wanamuziki hao.

Baadhi ya wasanii hao ni mwanadada DJ Kezz, mabarobaro Jose Kaleson, Sammy G, Presenter Kai kati ya wengine wengi.

DJ Kezz, jina lake halisi likiwa Keziah Jerono, ameibukia kuwa maarufu sana katika siku za hivi karibuni kutokana na utunzi wake wa nyimbo wa kipekee.

Yeye ni mwanachama wa kundi la muziki la Msanii Group (la Kanisa la Kiadventista-SDA), ijapokuwa ameanza utunzi wa kipekee, ulioibukia kupendwa na vijana wengi.

Kutokana na utunzi wake, wengi wanamtaja kama ‘Gloria Muliro wa kizazi cha sasa’.

Akiwa na umri wa miaka 24 pekee, amefanikiwa kushirikiana na baadhi ya wanamuziki kama Benachi, Rose Muhando, Timeless Noel, Didiman, Guardian Angel kati ya wengine wengi.

Kwa sasa, anatamba kwa vibao kama ‘Kilele’ na ‘Badilika’ alivyowashirikisha wanamuziki Benachi na Rose Muhando mtawalia.

Mwanamuziki Jose Kaleson anatajwa kuwa ‘Willy Paul wa kizazi cha sasa’. Sababu ni kuwa, wanafanana na mwanamuziki huyo kama shilingi kwa ya pili. Pia, utunzi na sauti zao zinafanana.

Baadhi ya vibao vyake vinavyosifika ni ‘Dawa’ na ‘Zamu Yangu’, aliomshirikisha chipukizi mwenzake, Sammy G.

Anasema kuwa “huu ni mwanzo tu wa kurejesha injili ilikokuwa”.

“Sisi ni mabalozi wa Mungu kuirejesha injili mahali ilipokuwa,” akasema.

Sammy G, naye alipata umaarufu aliposhirikishwa na msanii Guardian Angel kwenye wimbo wake ‘Nimependa’ miezi minne iliyopita. Ni barobaro aliye na umri wa miaka 23 pekee.

Kufikia sasa, wimbo huo una mitazamo zaidi ya 8.9 milioni katika mtandao wa YouTube.

Chipukizi huyo anasema “hataangalia nyuma”.

Mwanamuziki Presenter Kai naye anajiita “balozi wa kuinua na kurejesha tena injili” kama ilivyokuwa katika miaka ya hapo nyuma.

Kwa sasa, anatamba kwa kibao ‘Ni Neema’ alichotoa miezi miwili iliyopita.