Chitembwe alilia kazi ya Maraga akihojiwa

Chitembwe alilia kazi ya Maraga akihojiwa

Na RICHARD MUNGUTI

MCHAKATO wa kumsaka Jaji Mkuu atakayechukua mahali pa Bw David Maraga ulianza Jumanne huku mwaniaji wa kwanza wa kiti hicho akidondokwa machozi mbele ya jopo la mahojiano.

Jaji Said Juma Chitembwe alijawa na hisia na kusita kujibu maswali alipoulizwa kuhusu kesi iliyomkabili 2011 ya ufisadi kuhusu Sh1.2bilioni. Jaji Chitembwe aliyeachiliwa katika kesi hiyo alisema alikuwa amesingiziwa na ilimchukua muda mrefu kujinasua na kusafisha jina lake.

Jaji huyo anayehudumu katika mahakama kuu ya Milimani jijini Nairobi alieleza tume ya kuajiri watumishi wa idara ya mahakama (JSC) kwamba, endapo atateuliwa kuwa Jaji Mkuu, atahakikisha kesi zinakamilishwa kwa muda usiozidi miezi sita.

“Je ulipata funzo gani uliposhtakiwa kwa ufisadi wa Sh1.2bilioni ulipokuwa umeajiriwa katika NSSF,” Kamishna Everlyne Olwande alimwuliza Jaji Chitembwe. Ni wakati huo Jaji Chitembwe alisita kujibu swali hilo na sauti yake kufungika huku machozi yakimtiririka.

“Ni vizuri umeniuliza swali hiyo. Nilipata mafunzo mengi mojawapo kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi za uhalifu katika muda unaofaa kwa vile washukiwa huteseka na kuumia. Funzo nililopata niliposhtakiwa ni kwamba, kesi zapasa kuamuliwa kwa upesi ndipo washukiwa wajue hatma yao,’ akaeleza nguvu zilipomrudia.

Akijibu maswali kutoka kwa Kaimu Jaji Mkuu Philomena Mwilu, Jaji Chitembwe alisema kile atakachozingatia ni kushirikiana na watumishi wote wa idara ya mahakama ndipo wananchi wanufaike.

Kuhusu uimarishwaji wa uhusiano kati ya asasi nyingine za serikali, Chitembwe alisema atakuwa anashauriana na afisi ya Rais hadi kutegua kitendawili cha kutoapishwa majaji 41 walioteuliwa na JSC mwaka uliopita.

You can share this post!

MKU kwenye mstari wa mbele katika masuala ya michezo

Vigogo wapimana akili