Makala

CHOCHEO: Dakika ngapi kabla kushusha mzigo?

June 15th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

WANAWAKE na wanaume wametofautiana vikali kuhusu muda ambao mume anapaswa kuchukua kutekeleza tendo la ndoa.

Huku wanawake wakisema kwamba mume anapaswa kuchukua dakika zaidi ya kumi na mbili, wanaume hushikilia shughuli hii hutegemea mambo tofauti ikiwa ni pamoja na mazingira ambayo tendo linafanyiwa na makeke ya mwanamke.

Hata hivyo, wataalamu wanasema muda ambao mwanamume anafaa kuchukua kukamilisha shughuli hutegemea hali ya yake ya kisaikolojia, anavyojiamini, hali yake ya afya na maandalizi kabla ya kipindi cha ngoma chumbani.

“Ni kweli kumekuwa na mdahalo kuhusu muda ambao mwanamume anafaa kuchukua kabla ya kushusha mzigo wakati wa tendo la ndoa. Ni kweli wanawake huwa wanatarajia mengi kutoka kwa wanaume wakati wa shughuli na ni kweli ni wanaume wachache wanaochukua muda wa zaidi ya dakika kumi kwenye burudani chumbani,” asema mtaalamu wa masuala ya mapenzi Jeremy Wambugu.

Anasema muda wa kawaida ambao mwanamume anapaswa kuchukua katika tendo la ndoa ni dakika sita.

“Kumekuwa na hekaya nyingi kuhusu muda ambao wanaume wanafaa kuchukua kutekeleza tendo la ndoa. Hekaya hizi zimepotosha watu na kuwafanya watarajie mengi kutoka kwa wachumba wao. Kwa sababu ya habari hizi na matarajio yasiyoweza kuafikiwa, ndoa nyingi zimevunjika wanawake wakilalama kwamba wanaume wao hawawaridhishi chumbani,” anaeleza mwanasaikolojia huyu.

Anasema tendo la ndoa ni sanaa ambayo utamu wake unatokana na maandalizi na utekelezaji wake na sio muda ambao mhusika mmoja anapaswa kuchukua. Hata hivyo wataalamu wanakiri kwamba wanaume wengi wamepungukiwa na nguvu za kula uroda na kushindwa kabisa kudumu hata kwa dakika moja kwenye shughuli.

“Tafiti zimeonyesha kuwa wanaume wengi wamepungukiwa na nguvu za kiume na kuwafanya wasidumu hata sekunde kumi kwenye ngoma chumbani. Hali hii husababishwa na mambo tofauti kama vile mitindo ya maisha, mfadhaiko, maradhi kama vile msukumo wa damu, kisukari na msongo wa mawazo,” aeleza Dkt Pinky Sohal wa shirika Love Care jijini Nairobi.

Kulingana na mtaalamu huyu wanaume hawana muda wa kufanya mazoezi na hata kujiandaa kwa tendo la ndoa wakiwa na wachumba au wake zao.

“Ukosefu wa maandalizi, mazoezi na mawasiliano kati ya wanandoa kumechangia wanaume kushindwa kujimudu wakati wa burudani chumbani na kushusha hata kabla ya wachumba wao kuridhika. Hii imekuwa ikiwaacha wanawake wengi wakitamani ngoma zaidi. Ajabu ni kwamba ni tatizo ambalo linaonekana kuwa na wanaume wa rika zote,” asema Dkt Sohal.

Wataalamu wanasema kwamba sababu ukosefu wa ubunifu na makeke kutoka kwa wachumba wao pia kunachangia hali hii.

“Mchango wa mwanamke kwenye shughuli unamchamgamsha mwanamume na kumtia ari na hamasa ya kushiriki ngoma. Makeke ya mwanamke huwa yanatia nakshi tendo la ndoa na mwamume anaweza kuchukua muda mrefu na pia kurudia raundi kadhaa,” aeleza.

Bw Wambugu anasema siri ya raha ni uhusiano wake na mtu wake.

“Wachumba wakiwa na uhusiano na mawasiliano bora, wanaelewana vyema bila ugomvi na mume akipata lishe bora na kufanya mazoezi, basi wanaweza kuridhishana bila kujali muda ambao mume anachukua kusoma katiba,” aeleza.

Nguvu zapungua

Wataalamu wanasema kote ulimwenguni, watu wamepungukiwa na nguvu za kula uroda na wanahusisha hali hii na mitindo ya maisha na mabadiliko ya teknolojia yanayonyima wachumba muda wa kufanya mazoezi na kuwa pamoja.

Kulingana na makala yaliyochapishwa kwenye jarida la Health Digest japo awali wanaume walikuwa wakipungukiwa na nguvu za kula uroda umri unaposonga, hali imebadilika huku wanaume wa kizazi cha sasa wakijikwaa kitandani na kufanya wanawake kuwapachika jina la wanaume wa kizazi cha sekunde tatu.

Wataalamu wanasema hakuna muda rasmi ambao mwanamume anafaa kuchukua kuridhisha mwanake chumbani bali inategemea ujuzi wa mtu wa kupandisha mzuka.