Makala

CHOCHEO: Dalili za hatari katika mapenzi

November 2nd, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

IKIWA uhusiano wako wa kimapenzi unakufanya ukasirike na kutokwa na machozi kila wakati, unafaa kuelewa kwamba mambo sio mazuri.

Na ikiwa tabia za mchumba wako zinakukosesha furaha, kukusononesha bure, basi usiwe king’ang’anizi, jitoe; tena haraka.

Wataalamu wa masuala ya mapenzi wanasema tabia zinazokosesha mtu furaha katika uhusiano hubadilika na kuwa maafa.

“Ni tabia kama hizi zinazofanya watu kuua wachumba wao. Hivyo basi, watu wanafaa kuwa waangalifu ili kuepuka maafa,” asema Daisy Wanjiku Kamau, mtaalamu wa masuala ya mapenzi katika kituo cha Love Care jijini Nairobi.

Kulingana na mwanasaikolojia huyu, tabia kama vile kupandwa na hasira kwa sababu ya mambo madogo, kukunyima uhuru wako na kukuchukulia kama mali yake binafsi, zinaweza kuzua maafa.

“Ukigundua kuwa mchumba wako anahisi kwamba anakumiliki sawa na mali yake nyingine kiasi cha kukunyima uhuru wa kufurahia maisha kama vile muda wa kujumuika na marafiki, kukunyima nafasi ya kujieleza na kukutaka kufuata maagizo yake kila wakati, basi unafaa kutahadhari na kuchukua hatua mapema ili kuepuka hatari inayoweza kutokea baadaye,” asema Bi Wanjiku.

Anashauri watu kukatiza uhusiano wakigundua wachumba wao wana tabia kama hizi kwa sababu walio nazo huwa vigumu kubadilika.

“Usisubiri hadi ujutie. Katiza uhusiano ukigundua kuwa mtu wako ana tabia zinazoweza kuweka maisha yako hatarini. Makosa ya wengi ni kukwamilia mtu kwa jina la mapenzi hata ikiwa tabia zake ni za kikatili,” aeleza.

Wataalamu wanasema wanawake na wanaume, wote wanaweza kuwa na tabia hii. “Wanawake wameua wachumba wao sawa na wanaume kwa sababu ya hasira, tuhuma na kukaidi maagizo yao,” asema.

Kulingana na mwanasaikolojia James Koome wa shirika la Independent Minds, watu wanafaa kuepuka wanaokosoa kila kitu wanachofanya au kusema. “Moja ya dalili kwamba mchumba anaweza kuwa hatari ni anapokosa kuona uzuri wowote katika ufanyalo na usemayo. Watu kama hao huwa wanataka kufanya wachumba watumwa wao kwa kila hali,” asema Dkt Koome.

Mtaalamu huyu anaeleza kuwa wenye tabia hizi huwa wanawashambulia wachumba hao kwa maneno ya kuwadhalilisha.

“Ikiwa hakuna unachosema au kutenda kinamfurahisha mchumba wako, basi kuna hatari,” asema.

Ugomvi mara kwa mara

Ugomvi wa mara kwa mara ni dalili nyingine ambayo wataalamu wanasema imekuwa ikizua maafa miongoni mwa wachumba.

“Ukigundua mchumba wako anapenda kuzua ugomvi kwa masuala madogo madogo, basi kuwa mwangalifu kwa sababu hana uvumilivu. Watu wenye hulka hii wanaweza kusababisha maafa,” aeleza Koome.

Wataalamu wanashauri kutonyamaza au kuwahadaa watu kuwa uhusiano wenu ni shwari ilhali hali si shwari.

“Kuna watu wanaonyamaza au kuficha wanayopitia mikononi mwa wachumha wao wakiogopa fedheha na unyanyapaa hadi pale maafa yanapotokea. Ni muhimu kuzungumza na unaowaamini ili uweze kupata msaada,” asema Koome.

Kilele cha tabia hizi ni mchumba kudharau mwenzake hadi anaanza kumnyima tendo la ndoa. Kulingana na wataalamu, kuacha kufanya mapenzi ni kunyima uhusiano wenu rotuba. “Kunyimana tendo la ndoa ni sawa na kunyima uhusiano chakula na maji ya kuukuza. Uhusiano kama huu huwa umekosa rotuba na katika hali hii, hukosa kunawiri na kushuhudia mizozo isiyokwisha,” asema Bi Wanjiku.

Bw Koome anasema ikiwa uhusiano wa mapenzi unakukosesha furaha, kukutenganisha na marafiki na jamaa zako wa karibu, basi kuwa makini na uchukue hatua usije kujuta baadaye.

Wanasaikolojia wanasema uhusiano wa mapenzi unapaswa kuwa wa furaha na sio mateso, dhiki moyoni na majeraha mwilini.