CHOCHEO: Hadaa ya mapenzi huja na kilio

CHOCHEO: Hadaa ya mapenzi huja na kilio

NA BENSON MATHEKA

Baada ya kuchumbiana kwa miaka mitatu, Kamau alimtaka Ciru ampeleke kwao wakapate baraka za wazazi wake ili wafanye harusi. Hii ilikuwa baada ya kumpeleka kwa wazazi wake kumtambulisha kama mpenzi na mke mtarajiwa. Hata hivyo, Ciru hakuchangamkia wazo la Kamau na akawa analihepa kila kimkumbusha.

“Nilishuku alikuwa akificha kitu lakini sikujua ni nini. Baadaye niligundua kwamba alikuwa amenidanganya hakuwa ameolewa na hakuwa na watoto ilhali ni mtalaka na mama ya watoto wawili,” anasema Kamau.

Anasema hakuamini Ciru alikuwa amemhadaa kwa miaka mitatu.

“Ni mwanamke mrembo aliyejaliwa umbo la kuvutia. Ni vigumu kugundua ni mama ya watoto wawili wa umri wa miaka 5 na 7,” akafunguka Kamau.

Barobaro huyu ambaye amefaulu katika biashara ni mmoja wa wanaume na wanawake wanaopagawishwa na mapenzi ya wachumba wanaokutana nao mijini wakijifanya hawajaoa au kuolewa ilhali ni waume, baba na wake wa watu.

“Ni mtindo unaoendelea sana hasa maeneo ya mijini ambako watu kutoka maeneo mbalimbali hukutana. Wanawake wanaacha waume zao nyumbani na wakifika mjini wanajikwatua na kuteka wanaume wakijifanya wanasaka wachumba. Vile vile, wanaume wanaacha wake na watoto wao mashambani na kuwachota wanawake mijini kwa madai bado singo,” asema Phylis Mwenda, wa shirika la Big Hearts, Nairobi.

Mwenda anasema inavunja moyo mtu aliyewekeza hisia, muda na mapenzi akidhani ameangukia mchumba wa ndoto yake kugundua kwamba alikuwa akitoka na mtalaka, mke, mama au mume wa mtu.

“Wanaodanganya huwa wajanja wanaotaka kuwatumia wanaume au wanawake. Huwa hawana nia ya kutaka kuoa au kuolewa,” asema Mwenda.

Vicky Irai, mwanadada mwenye umri wa miaka 27 anasema kwamba alipoteza miaka minne na mwanamume akidhani alikuwa amepata mchumba wa maisha yake na baadaye akagundua alikuwa mume na baba ya watoto watano wa karibu rika lake.

“Nilisongwa na mawazo, nilifadhaika kwa kuwa nilikuwa tayari na mimba yake,” asema.

Vicky asema alitamani atoe mimba lakini baada ya kupata ushauri nasaha, akabadilisha nia.

“Kwa sababu nilikuwa na kazi nzuri, niliamua kuzaa mtoto wangu. Nilimuacha jamaa huyo na nilipompata mume wangu wa sasa, nilimweleza ukweli kwamba nilikuwa mama wa mtoto mmoja ambaye baba yake tulitofautiana na tukaachana,” akasema Vicky.

Kulingana na Dennis Wanyama, mwanamume mwenye umri wa miaka 36, aligundua mkewe aliyehamishwa hadi mjini kikazi, alikuwa akidanganya watu hakuwa ameolewa. “ Nilimtembelea mjini na kushangaa kufahamu alikuwa akiambia watu alikuwa singo,” asema.

Mwenda anasema watu wanafaa kueleza wanaowamezea mate ukweli. “Anayekupenda kwa dhati hatakukataa, anafaa kukupenda ulivyo. Ukweli unaweka mtu huru. Ili kujiweka huru, usiingie katika majaribu ya kudanganya wanaokumezea mate,” asema.

Wataalamu wanasema kwamba mtu anayetaka kuolewa au kuoa, anayempenda mume au mke wake, huwa hafichi maisha yake ya mapenzi.

Malit Tumaaina, mfanyabiashara mwenye umri wa miaka 30 anasema kwamba nusura aangamizwe na mume wa mwanadada aliyekuwa akimmezea mate.

“Tulikutana katika shughuli za kibiashara na akanichangamkia. Ni mrembo wa kutamaniwa na nikadhani nilikuwa nimeangukia mchumba mwenye sifa ninazotaka. Baadaye mumewe alipashwa habari na kunijia kwa fujo akinilaumu kwa kuchepuka na mke wake,” aeleza Malit.

Kulingana na Shadrack Mugambi Ntuai wa shirika la Abudant Love, watu wengi wamekuwa wakijipata mashakani kwa kuchumbia watu wanaowadanganya hawajaolewa au hawana watoto.

“Kuna wanaosubiri unazaa nao kisha wanakweleza wana watoto au wake wengine. Hii imekuwa ikisababishia watu msongo wa mawazo na mfadhaiko. Baadhi ya watu wamekuwa wakichukua hatua hatari,” asema.

Mugambi anashauri watu kuwa makini na uwazi katika masuala ya mapenzi.

You can share this post!

DOUGLAS MUTUA: Polisi pia ni watu, watunzwe ndipo wapate...

Wanasiasa wakerwa na matamshi ya Junet Mohamed