Makala

CHOCHEO: Harusi inapoteleza…

December 19th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

KWA miaka minne ambayo Aisha alikuwa mchumba wa Salim, alikuwa na furaha ambayo kila mtu hutamani katika uhusiano wa mapenzi.

Lakini walipotangaza harusi yao, mambo yalianza kubadilika. Sio kwa sababu ya Salim, bali changamoto walizopata hadi akadhani harusi yao haingefanyika.

“Tulikabiliwa na wakati mgumu wakati wa kuandaa harusi yetu. Baadhi ya changamoto zikitoka kwa jamaa zetu wa karibu na hata marafiki. Ilifikia hatua ambayo nilimwambia Salim tutoroke tukaishi mbali kama mume na mke bila nikaha rasmi,” asema Aisha. Hata hivyo, Salim alikataa, wakakabiliana na visiki vyote hadi wakafanya harusi ya kufana.

Kwa Pat, ni wakwe na mashemeji watarajiwa waliokuwa wakimwekea vizingiti alipotangaza nia ya kumuoa binti yao aliyekuwa amemchumbia kwa miaka sita. “Niliwekewa masharti makali ambayo Brenda hakufurahia. Niliambiwa mambo kumhusu yeye na familia yake ambayo kama singekuwa nampenda kwa dhati, ningebadilisha nia. Nilijikaza kama mwanamume na kumuoa kiosha roho wangu kwa harusi ya nguvu sana na sasa tunaishi kwa furaha,” asema Pat.

Baadhi ya vizingiti, huwekwa na viongozi wa kiroho jinsi alivyoshuhudia Myra alipoenda kumuomba pasta wa kanisa lake ushauri kuhusu ndoa. “Niliyoyasikia kutoka kwa pasta huyo sikuweza kuamini yalitoka kwa kinywa cha kiongozi wa kiroho. Siwezi kuyatamka. Yaliniuma sana na nilipokataa kutimiza aliyotaka, alikataa kuongoza harusi yangu,” asema Myra.

Washauri wa wanandoa wanasema kuwa vizingiti wanavyopata wachumba wanapopanga harusi huwa ni mtihani wa kupima upendo wao. “Japo baadhi ya vizingiti huwa vinasababishwa na watu wenye nia mbaya, huwa ni mtihani kwa wanaopanga ndoa. Kwa mfano, ikiwa vinawekwa na jamaa wa karibu, vinakufanya kuwaelewa vyema na kukuwezesha kupanga jinsi ya kuhusiana nao,” asema Steve Kiano wa kituo cha Liberty mjini Athi River.

Anasema kwamba baadhi ya watu huwa wanapata vikwazo kutoka kwa wazazi wao wakati wa kupanga harusi. Delphina Wangui mkazi wa mtaa wa Syokimau, Nairobi anasema alikuwa na wakati mgumu kuwashawishi wazazi wake kupokea mahari kutoka kwa mpenzi wake.

“Walikuwa wakimfahamu James kwa miaka mitatu. Lakini wakati tulipotangaza mipango ya kufanya harusi, walianza kisirani. Hawakuwa na sababu maalumu ya kukataa kutupatia baraka tufunge ndoa. Ilinibidi nitume wazee wa familia kumshawishi baba yangu na pia aliwatatiza sana. Alikubali kupokea mahari wazee walipotisha kumtenga,” alisema Wangui.

Viongozi wa kidini walaumiwa

Kiano analaumu viongozi wa kidini wanaowavunja moyo wachumba wanaotaka ushauri kuhusu ndoa.

“Wapo wanaofanya hivyo kwa sababu za kibinafsi, kuna wengine wanaofanya hivyo kwa sababu ya tamaa kama vile kuitisha pesa nyingi kufungisha harusi. Kuna wanaokataza waumini kusaidia vijana wa makanisa wanapopanga harusi na kuna wanaohisi kuwa watapoteza washirika wasichana wakiolewa. Haifai kuwa hivi. Jukumu la viongozi wa kidini ni kuwaelekeza wachumba kuoana katika ndoa takatifu na sio kuwawekea vikwazo,” asema.

Watalaamu wanasema vikwazo vingine vinavyotokea wakati watu wanapoanza kutayarisha harusi huwa vya kifedha.

“Unapata hali ambayo hukutarajia. Pesa zinakosa na kutishia mipango ya harusi dakika ya mwisho. Hali hii ikitokea, wachumba wanafaa kuketi na kurekebisha mipango yao kwa kupunguza bajeti yao,” asema Faith Kimondo wa shirika la Do It Right, jijini Nairobi.

Anashauri wanaopanga harusi kujiandaa kwa visirani, visiki na vibwanga vya kila aina. “Kufikia siku ya harusi, watu huwa wanakumbana na changamoto za kila aina. Muhimu ni kujipa moyo ili kupata mke na mume wa ndoto yako. Visiki hivi vinaweza kutoka popote na kwa yeyote wakati wowote wa kuandaa harusi,” asema Faith.