Makala

CHOCHEO: Jipu la ndoa

October 5th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

TALAKA imekuwa kawaida siku hizi.

Wanandoa wanachokana na kuwasilisha kesi za talaka kisha kuanza kuvutana sababu ya mali.

Wengi wanataka posho kutoka kwa waliokuwa wachumba wao na wengine wanavutana kuhusu watoto.

Wataalamu wanasema japo ni haki ya kila mwanandoa kuwasilisha kesi ya talaka akishindwa kuvumilia, idadi ya ndoa zinazovunjika zikiwa changa inatia hofu.

Kulingana na wanasaikolojia, idadi ya watu wanaovunja ndoa zao wakiwa na umri wa miaka 30 inazidi kuongezeka.

“Katika umri huu, watu wanapaswa kuwa wakifurahia ndoa zao, wakijenga familia, kutafuta mali na kujiandaa kwa hali ya baadaye. Ni kipindi ambacho wanafaa kuwa wakipata na kulea watoto lakini inasikitisha wengi wanatafuta talaka,” asema mwanasaikolojia David Solu wa shirika la Big Hearts jijini Nairobi.

Mtaalamu huyu anasema tofauti na miaka ya awali, wanandoa walipokuwa wakiogopa unyanyapaa unaotokana na talaka hasa katika jamii za kiafrika, talaka sasa ni sawa na mtindo wa maisha.

“Haikuwa rahisi mtu kufikia uamuzi wa kuomba talaka. Watu waliogopa aibu ya kutalikiana lakini sasa hali imebadilika na imekuwa kawaida wanandoa kuachana,” asema Bw Solu.

Wataalamu wanahusisha hali hii na ndoa za mapema na pia ukosefu wa maandalizi ya ndoa.

“Vijana wanakimbilia ndoa bila kufahamiana, wanaoana hata kabla ya kujuana vyema na kabla ya kukomaa na wakifikisha umri wa miaka 30, huwa wanachokana na kutambua kwamba wamekuwa wakiishi na watu ambao hawawezi kutimiza ndoto zao za maisha,” asema.

Dkt Sue Kamau, mtaalamu wa masuala ya mapenzi, anaongeza kuwa hali hii pia imetokana na kwamba wengi wanafahamu haki zao kinyume na ilivyokuwa awali.

“Hii inachangia ongezeko la talaka ndoa zingali changa. Pia imefanya watu wengi kuogopa harusi na kuamua kuishi singo badala ya kuolewa kisha ndoa ivunjike wakati ambao wanaihitaji zaidi,” aeleza.

Aidha kuna wanaohoji kuwa mabadiliko ya kiteknolojia yanachangia pakubwa talaka miongoni mwa wanandoa wachanga.

“Kila uchao, kuna ripoti za wanandoa wanaotofautiana kwa sababu ya mitandao ya kijamii, simu za mkono na hata vipindi vya runinga. Teknolojia imekuwa tishio kubwa kwa ndoa changa,” aeleza.

Bi Kamau anakubaliana naye akisema wanandoa wengi wa kizazi cha sasa wamekuwa wakiiga wanayopata kwenye mitandao, jambo linalosababisha ndoa kuvunjika.

“Ni kweli watu wengi wameelimika, ni kweli wanafahamu haki zao kuliko waliowatangulia lakini tishio kubwa kwa ndoa siku hizi ni teknolojia hasa mitandao ya kijamii,” asema Bi Kamau.

Kulingana na Pasta Derrick Kariuki wa kanisa la Liberty Center, Athi River, idadi ya talaka ndoa zikiwa changa inatokana na watu kutumia njia za mkato kufunga ndoa.

“Watu hawataki ushauri kabla ya ndoa. Wanaoana kabla ya kufahamiana vyema. Kuna wale wanaoingia katika ndoa bila kuwa na nia njema na kuna wale ambao matarajio yao katika ndoa hayatimizwi kisha wanaamua kupata talaka mapema badala ya kupoteza muda bure wakisubiri kusuluhisha mambo,” asema.

Uhuru

Wataalamu wanakubaliana kuwa ndoa siku hizi zinavunjika kwa sababu watu wengi wanaamini kuolewa kunawanyima uhuru wao.

“Wengi siku hizi na hasa wanaoingia katika ndoa mapema huwa wanahisi kuwa zinawafunga na wanaamua kutafuta talaka ili wajifungue na kupata uhuru wao,” aeleza Bi Kamau.

Wanasaikolojia wanasema kuwa watu wanaofunga ndoa baada ya kutimiza miaka thelathini, wanaopata mafunzo kutoka kwa wataalamu waliohitimu na wanaochumbiana kwa muda mrefu, huwa sio rahisi kutalikiana.

“Ndoa ni zaidi ya ustadi wa kulishana uroda wanavyoamini vijana wengi. Inahitaji kupaliliwa kabla na baada ya kuoana. Ndoa inahitaji uvumilivu ambao wengi siku hizi hawana,” asema Pasta Kariuki.