Makala

CHOCHEO: Kuchokana katika ndoa

August 30th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

IKIWA umeoa na shughuli za chumbani zimeanza kupungua, hiyo ni dalili kwamba mumeanza kuchokana na ndoa inaeleka kuvunjika.

Wataalamu wanasema tendo la ndoa husaidia kuimarisha uhusiano kati ya wanandoa.

Hata hivyo wanasema kuwa uthabiti wa ndoa haufai kujengwa katika tendo la ndoa pekee. “Moja ya dalili za ndoa inayoelekea kuvunjika ni kupungua kwa shughuli chumbani bila sababu maalumu. Kule kuhisi kuchoka na mwenzako ni ishara kuwa nguzo ya ndoa imeanza kuwa dhaifu,” aeleza mwanasaikolojia David Mwangi wa shirika la Liberty Live Center, jijini Nairobi.

Anasema hii haswa ni kwa wanandoa barobaro ambao wana nguvu na damu moto.

Wataalamu wanasema tendo la ndoa huwa linaunganisha hisia na mwili, uhusiano huvunjika wakianza kukaushana chumbani.

Akiandika katika jarida la mtandaoni la Huffing Post, mwanasaikolojia Sarri Cooper alisema kukosa kufanya tendo la ndoa hufanya mume au mke kuhisi upweke na kutengwa.

Mtaalamu huyu anasema wanaofika kwake wakiwa na tatizo hili huwa anawashauri kuzungumzia suala lenyewe.

Kulingana na Mwangi, wanandoa hujipata wakichokana na kukaushana chumbani kwa sababu ya kukosa kuwasiliana vyema. “Mawasiliano yanapovunjika katika ndoa, huwa ni vigumu wachumba kuchangamkiana na wanaofika kwa wataalamu, hatua ya kwanza huwa ni kuwasaidia waanze kujadili masuala haya bila kurushiana lawama,” aeleza.

Mtaalamu huyu anataja tuhuma kama dalili nyingine ya ndoa inayoelekea kuvunjika. “Tuhuma huzaa ugomvi na wanandoa wakianza hulka hii, kitumbua chao huwa kimeanza kuingia mchanga. Lawama ni sumu kwa ndoa. Matatizo yanapoibuka, yanafaa kujadiliwa katika mazingira ya kuelewana na sio kulaumiana,” aeleza.

Dkt Susan Wamwende wa shirika la Love Care jijini Nairobi anasema kuwa lawama hasa kuhusu tendo la ndoa zinaweza kuvunja ndoa haraka sana. “Kila mchumba na hasa wanawake hupenda kutamaniwa. Mtu akihisi kutamaniwa, huwa anachangamka na kusisimka lakini akihisi kupuuzwa hugeuka baridi chumbani,” asema.

Kwenye makala yaliyochapishwa katika gazeti la New York Times, mtafiti wa masuala ya tendo la ndoa Marta Meana alisema mtu akikosa kuhakikishia mchumba wake kuwa anampenda na kumtamani kimapenzi, basi tayari nyufa huanza kujitokeza.

Kulingana na Marta dalili nyingine ya ndoa kusambaratika ni wanandoa kukosa kuaminiana. “Imani ya mtu kwa mume au mkewe ni moja ya nguzo za ndoa na ikikosekana, hakuna ushirika wowote,” aeleza.

Akiunga mkono kauli hiyo, Dkt Wamwende anasema; “mtu anaweza kukosa imani na mchumba wake akigundua ana mipango ya kando, au anamficha masuala muhimu hasa ya kifedha. Wanandoa hawafai kwendeana kichini chini na kufichana mambo. Tabia hiyo ikianza, ndoa huwa inaelekea ukingoni,” aeleza.

Utatuzi upo

Ingawa watu wengi hutaja kukosa kuridhishana chumbani kama dalili na sababu ya kuvunjika kwa ndoa, wataalamu wanasema ni suala linaloweza kutatuliwa wachumba wakiwa na mawasiliano mema.

“Tatizo ni pale mmoja anapotumia suala hilo kumdhalilisha na kumdharau mwenzake. Kufanya hivi kunaweza kuvunja ndoa,” asema Mwangi.

Kulingana na Dkt Wamwende, wengi wamevuruga ndoa zao kwa kukaziana asali.

“Kumpuuza mchumba wako anapokufeel, kunamfanya kuhisi kwamba haumpendi na kunaweza kuyumbisha ndoa yenu,” aeleza.

Kwenye kitabu chake The Power to Mindful Love & Sex, mwanasaikolojia Avina Cadel anasema kwamba mtu hafai kumpuuza mchumba wake hasa anapopandwa na hanjamu.

“Inafaa watu wajadiliane kuhusu mbinu za kuchangamshana chumbani na hata masuala ya kifedha ikiwa wanataka kudumisha uthabiti wa ndoa yao,” aeleza.