Makala

CHOCHEO: Kumbania unyumba ni kualika vidudumtu

October 24th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

KWA miaka sita ambayo Eric amekuwa katika ndoa, hakuwa amemshuku mkewe Tabby.

Mwanadada huyo alikuwa akimheshimu na kukidhi mahitaji yake ya tendo la ndoa kikamilifu hata baada ya shughuli kuongezeka nyumbani alipojaliwa kifungua mimba.

Hata hivyo, matukio ya miezi minane iliyopita yamemfanya kuwa na wasiwasi. Anasema kwamba Tabby alibadilisha tabia, alianza kufika nyumbani akiwa amechelewa na kudai alikuwa na kazi nyingi ofisini madai ambayo Eric alishuku.

“Alianza kufika nyumbani baada ya saa moja jioni licha ya kuwa anafanya kazi katika ofisi ya serikali inayofungwa saa kumi na moja. Ofisi yao iko kilomita mbili kutoka nyumbani. Ameanza kunibania tendo la ndoa, mara anadai amechoka au anahisi usingizi na mazungumzo pia yamepungua. Ninashuku amepata kituliza roho huko nje,” asema Eric.

Kulingana na mwanamume huyo, mkewe ameacha kuwasiliana naye jinsi alivyokuwa akifanya na huwa anashinda akichati kwenye simu yake.

“Wakati mwingine huwa analala saa saba usiku akiwasiliana na watu ambao siwafahamu. Hilo, pamoja na kunibania tendo la ndoa, ni ishara kwamba anagawa tunda. Kwa nini aninyime haki yangu ya chumbani ikiwa hana mipango ya kando?” anahoji Eric.

Deborah Kanyi, ambaye amekuwa katika ndoa kwa miaka minne ana lawama sawa na Eric. Anasema mumewe Peter ameanza tabia ya kumbania uroda akidai amechoka. “Alikuwa akinipa burudani tosha lakini siku hizi amelegea. Pia anafika nyumbani usiku kabisa akidai huwa na shughuli nyingi na hataki nishike simu yake,” asema.

Kulingana na wanasaikolojia na washauri wa masuala ya ndoa, mtu akianza kumnyima mpenzi wake tendo la ndoa bila sababu maalumu, anaweza kuvuruga ndoa yake.

“Kubadilika ghafla na kuanza kumnyima mchumba wako tendo la ndoa kunaweza kufanya uhusiano wenu kuwa baridi. Vilevile, uhusiano ukiwa baridi unaweza kufanya mmoja wenu kutochangamkia tendo la ndoa. Hali kama hii inaweza kusuluhishwa kupitia mazungumzo ya wazi katika mazingira ya kuheshimiana,” asema Serah Karimi, mtaalamu wa wanandoa katika shirika la Forever Care, jijini Nairobi.

Ikiwa anayelaumiwa anakataa kufanikisha mawasiliano kama vile kutochukua simu au kukataa mazungumzo, huwa anampa mwenzake sababu za kuamini ana kimada anayemtuliza nje ya boma lake.

“Kuna tabia ambazo walio na mipango ya kando huwa nazo kama vile kutowachangamkia wachumba wao wakati wa tendo la ndoa. Hii huwa inasambaratisha uhusiano au kuufanya baridi kiasi cha kukosesha mtu raha,” asema.

Washauri wa ndoa wanasema kwamba wanandoa hawafai kubaniana tendo la ndoa ikiwa hali inaruhusu. “Jimwage mzima mzima kwa mtu wako. Mpe haki yake. Mke akitaka mpe, mume akitaka mpe, wakati wowote. Hii itaimarisha raha katika ndoa. Ukianza vijisababu, utakuwa unajipalilia makaa na kuchoma uhusiano wetu. Mchangamkie mtu wako bila mipaka,” asema Karimi.

David Kamau, mshauri wa wanandoa katika kanisa la Liberty Live Center, mjini Athi River, anasema kwamba mtu anapoanza kumbania au kumnyima mwenzake tendo la ndoa bila sababu maalumu, huwa anakiuka jukumu lake.

“Tendo la ndoa ni haki muhimu inayounganisha wanandoa. Hivyo basi, kumnyima mwenzako bila sababu maalumu, ni kuvunja ile nguzo ya ndoa,” anasema Kamau.

“Ushauri wangu ni kutoa mwili wako bila vikwazo kwa mwenzio,” asema.

Karimi anasema ingawa kuanza kuchelewa kufika nyumbani, kutochangamkia ngoma chumbani na kutotaka kuwasiliana na mchumba wako huwa ni ishara mtu ameanza michepuko, ni muhimu kuthibitisha kwanza kabla kukurupuka.

“Inaweza kuwa mtu wako anasema ukweli akikuambia amechelewa kazini au amechoka. Lakini hii haiwezi kuwa ni kila wakati au kwa siku fulani. Haiwezi kuwa ni kila Ijumaa au wikendi. Ikianza kuwa kawaida, basi una sababu ya kushuku lakini muhimu ni kuthibitisha kwanza,” asema.

Kulingana na Kamau, kumbania mchumba wako tendo la ndoa sio tu kukiuka sheria za ndoa mbali pia ni kumtia katika majaribu. “Mwandalie mtu wako burudani, mtimizie haki yake ya ndoa, mchangamshe ahisi raha naye hatakushuku,” asema.