CHOCHEO: Kumchongoa sawa na kuchongea penzi lenu

CHOCHEO: Kumchongoa sawa na kuchongea penzi lenu

Na BENSON MATHEKA

“MBONA huwezi kuwa kama mume wa Njoki ambaye hushinda na watoto wake na kumthamini mkewe?” Hii ilikuwa mara ya kumi Wangui kumlinganisha mumewe Teddy na waume wa wanawake wengine jambo lililomkwaza sana.

Ni sawa na anayopitia Lilian ambaye mumewe huwa anamlinganisha na wanawake wengine mtaani na anaowaona kazini au kukutana nao katika hafla mbalimbali.

“Ananichosha na akiendelea, nitamwambia aende akaishi nao au niondoke nimpatie nafasi ya kuchagua anayehisi anamfaa. Sitaendelea kuvumilia mchongoano wake kila siku,” asema Lilian.

Kwa Cindy, mumewe amekuwa akimtaka avalie kama wanawake wengine ilhali ni mitindo isiyomfurahisha.

“Patrick anataka niwe kama wanawake wengine. Kila wakati anasifu mitindo yao ya mavazi na nywele ambayo hainipendezi,” asema.

Cindy anashuku kuwa mumewe anachepuka na wanawake wengine anaoshinda akiwasifu.

Kulingana na wataalamu wa masuala ya mapenzi, ni makosa kumchongoa mchumba wako kwa vyovyote vile au kumlinganisha na mwanamume au mwanamke mwingine.

“Kufanya hivi kunamfanya ahisi kuwa haumpendi au mapenzi yako kwake yamepungua. Anaweza kutilia shaka uaminifu wako katika uhusiano wenu,” asema Stephen Karanja, mshauri mwandamizi katika shirika la Love Care jijini Nairobi.

Karanja anasema kwamba badala ya kumchongoa, au kumlinganisha mpenzi wako na mwanamume au mwanadada mwingine, unafaa kumsaidia na kumbadilisha awe utakavyo.

“Ikiwa ni mtindo wa nywele, hakikisha umemfadhili badala ya kumwambia fulani anapendeza. Ikiwa mtindo huo haumpendezi, usimlazimishe, kuna mingine inayoweza kumtoa vyema ikuvutie pia. Cha muhimu ni kuheshimu uamuzi wa mtu wako kwa sababu haukumpenda kwa kuwa alikuwa akifanana na unaomlinganisha nao,” asema Karanja.

Bezo na dharau

Wataalamu wanasema kuna wanaohisi wachumba wao wameanza michepuko wanapowalinganisha na wengine.

“Si lazima anayekulinganisha na mtu mwingine awe na mpango wa kando japo kuna uwezekano mkubwa wa kuchepuka akipata nafasi hiyo,” asema na kuongeza kuwa kuna wale ambao lengo lao huwa ni kuwahimiza wachumba wao kujiweka katika hali ya kuvutia.

Kulingana na Hellena Kwita wa shirika la Big Hearts jijini Nairobi, wachumba wanafaa kusaidiana kujiimarisha katika kila hali pasipo mchongoano, kubezana au dharau.

“Unapolinganisha mtu wako na mwingine kwa hali yoyote ile, unaonyesha unamdharau. Ni ishara ya mapungufu katika uhusiano wenu. Mnafaa kusaidiana na kujengana. Mapenzi ni kufanya mtu wako kuwa bora kila siku pasipo kuumizana moyo. Daima usimfananishe au kumlinganisha mtu wako na mwingine. Utabomoa penzi lenu na kuporomosha uhusiano wenu,” asema Kwita.

Cecilia Ambani, mwanadada mwenye umri wa miaka 32, asema alimbadilisha mumewe kuwa atakavyo bila kumlinganisha na mwanamume mwingine.

“ Nikiona mwanamume na suti nzuri, huwa nampeleka mume wangu dukani kujipima na ikimtoa vyema, namnunulia au namwambia anunue tukiwa na pesa. Simwambii niliona fulani akiwa ameivaa,” asema.

Wataalamu wanasema watu wengi wanavunja uhusiano wa mapenzi na hata ndoa zao kwa sababu ya tamaa. “Kuna wanaoongozwa na tamaa na hao ni rahisi kuchepuka au kuacha wapenzi wao baada ya kuwalinganisha na watu wengine hasa pale wanaowafananisha nao ni watu wenye mali, warembo au elimu au kazi nzuri,”asema Karanja.

Anasema watu wanafaa kubaini ukweli kuwa macho hayana pazia na sio kila wanachoona wanafaa kuiga.

“Hakuna wakati binadamu watatoshana au kufanana. Huu ndio urembo wa dunia. Yaani watu wa sura, umbo kimo, saizi na matabaka mbalimbali. Juhudi na bidii ni muhimu lakini wapenzi hasa walio katika ndoa hawafai kulinganisha watu wao na wengine isipokuwa pale ambapo waonekana bora kuliko hao wanaofananishwa nao. Na hata hivyo, hawafai kuwabeza au kudharau watu wengine kwa kuwa uwezo wa watu ni tofauti,” aeleza Karanja.

You can share this post!

FUNGUKA: ‘Sauti nyororo huniyeyusha mzima’

MWANAMUME KAMILI: Lau wangalijua utamu wa kuvivalia viatu...