Makala

CHOCHEO: Kutafsiri ndoto za mapenzi

July 12th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

UKIPATA ndoto ya mapenzi au ukiota ukifanya mapenzi na mtu asiye mpenzi wako, usikimbie kumweleza.

Japo wataalamu wa masuala ya mapenzi wanasema ndoto nyingi za kufanya mapenzi zinaweza kuimarisha uhusiano wa mtu na anayemuota, wanatahadharisha kuwa inaweza kuwa na maana tofauti.

“Kwa mfano mtu anaweza kuota akifanya mapenzi na mfanyakazi mwenzake ambaye hajawahi kuwa na hisia za mahaba kwake au kumtamani maishani mwake. Ndoto kama hii huwa na maana uhusiano wao wa kikazi utaimarika zaidi na wala sio kwamba wawili hao wanapaswa kuwa wapenzi,” aeleza mtaalamu wa ndoto Suleiman Soraya.

Anasema kwa watu wengi, ndoto za mapenzi huwa zinahusisha watu wanaowafahamu katika maisha yao ya kila siku.

“Ikiwa mtu unayeota ukifanya mapenzi naye sio mpenzi wako au umekuwa ukimmezea mate na hajameza chambo, usiende kumweleza ulivyoota. Unaweza kuaibika sana iwapo huyo hana hisia za mapenzi kwako,” aeleza Soraya.

Kwa jumla, mtaalamu huyu anasema ndoto za mapenzi huashiria kwamba anayeota anajali anayemuota.

“Ndoto nyingi za mapenzi zinaweza kumaanisha kuwa mtu anahitaji furaha katika maisha yake na anayeota anaweza kuchangia hali hiyo kwà njia tofauti. Kitendo cha kuwa katika uhusiano wa mapenzi katika ndoto kinaweza kumaanisha kuwa unahitaji furaha katika maisha yako na kukuelekeza kwa mtu ambaye kwa njia moja au nyingine anaweza kukusaidia kupata furaha hiyo,” aeleza Soraya.

Anasema watu wengi huwa wanapata ndoto za mapenzi na wapenzi wao uhusiano ukiwa mchanga. Hata hivyo anaonya kuwa ndoto za mapenzi zinaweza kufanya mtu kumtawala mwenzake akihisi anampenda zaidi na kwa kufanya hivi kuharibu uhusiano wao.

Kulingana na watafiti wa ndoto, mtu akiota akijivinjari na mpenzi wake inamaanisha anajali maisha yake ya ndoa na familia ni yenye furaha au akiwa na mpenzi huyo wanaweza kuwa na uhusiano na familia yenye furaha.

Mtafiti wa ndoto Howard Dean naye anasema kwamba mtu akiota akifanya mapenzi na mtu wake inamaanisha uhusiano wao unahitaji kupaliliwa zaidi.

“Ikiwa uko katika uhusiano wa kimapenzi na mtu na uote mkifanya mapenzi sebuleni au katika nyumba yenu iliyopambwa, inamaanisha unaweza kumposa na hatimaye awe mke au mume wako,” asema na kuongeza kuwa mazingira ya ndoto ndiyo huwa yamesitiri maana yake.

Dean anasema mtu akiota na mtu ambaye sio mpenzi wake ni kumaanisha kuna hulka ya mtu huyo inayomvutia.

Mvuto

Anasema kuwa mtu akiota akiwa na uhusiano wa kimapenzi na watu maarufu au mashuhuri huwa inamaanisha kuna hulka ya watu hao inayomvutia.

“Ajabu ni kwamba baadhi ya watu huwa wanasononeka baada ya kupata ndoto za mapenzi na watu wasioweza kuwakaribia au ambao ni wa hadhi ya juu kuwaliko. Mtu anafaa kutafuta maana ya ndoto kwa kupata tafsiri kamili,” asema Soraya na kuongeza kuwa ndoto za mapenzi zinaweza kupatia mtu furaha au huzuni.

Wataalamu wanasema baadhi ya ndoto za mapenzi zinaweza kuwa ishara kuwa mtu anahitaji upendo zaidi kutoka kwa anayemuota. Zinaweza pia kumaanisha mtu anahitaji kujipeleleza yeye mwenyewe badala ya kujilinganisha na anayeota wakihusika kwenye mapenzi.

“Uhusiano wa mapenzi hujengwa na watu wawili na kuna ndoto za mapenzi zinazomaanisha mtu anafaa kutoa mchango wake kikamilifu kujenga uhusiano wao,” asema Soraya.