Makala

CHOCHEO: Lo, sihadaike na nyama ya ulimi!

March 9th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

WANAWAKE wengi wamekuwa wakipagawishwa kimahaba na wanaume magwiji wa kusuka misitari.

Wanaamini kwamba wanaume kama hao wanajua mapenzi kuliko wale ambao ni wachache wa maneno.

Wanachosahau ni kuwa mingi ya misitari wanayorushiwa na wanaume huwa imepambwa kwa uongo.

“Vipusa wengi wamejuta baada ya kupagawishwa na misitari wanayorushiwa na wanaume baada ya kung’amua kwamba ilikuwa imejaaa ahadi za uongo. Kwa hakika, misitari hiyo huwa ni kinyume kabisa na tabia halisi ya anayeisuka, ” asema mtaalamu wa masuala ya mapenzi Emma Ambani wa kituo cha Love care jijini Nairobi.

“Chunga sana mwanamume stadi wa kutongoza wanawake. Utapata wengi wao huwa wanatoa ahadi za uongo kupitia maneno matamu ambayo huwa yanawazuzua vidosho na kuangukia mitego yao, ” asema Bi Ambani.

Anasema wengi wao huwa ni wanaume watundu wanaoelewa wanachotaka wanawake.

“Nyingi ya ahadi wanazowapa wanawake huwa hewa. Lengo lao huwa ni kuwanasa ili wachovye asali kisha wanawatema na kuwaacha wakisononeka. Ajabu ni kwamba wanawake wanawapenda zaidi,” aeleza.

Wataalamu wa mapenzi wanasema wale wanaoteseka zaidi ni wanawake wanaopanga kuolewa na wanaume wa aina hii.

Wanasema watu wengi wanaokubali kuolewa na wanaume kama hawa hujuta.

“Misitari inayorushwa watu wanapotafuta wachumba haifai kutumiwa kama msingi wa ndoa. Wanaokubali kuolewa baada ya kuahidiwa makuu na wachumba wao mara nyingi hujikuta majutoni,” asema mtaalamu wa mapenzi na mshauri wa wanandoa katika kituo cha Maisha Mema Richard Kamemchi.

Anasema kwamba maneno mengi ya kuvutia ambayo wanaume huwaambia vipusa huwa yanalenga kuwanyorosha wakubali kuwarusha roho pekee.

Anasema wanaume hutumia mbinu hi kwa sababu wanawake wamekuwa wakiwapa masharti makali kabla ya kuwafungulia mzinga wachovye asali.

“Siku hizi dunia imebadilika mno huku watu wengi wakiongozwa na tamaa… Watu wamekolewa na tamaa na imekuwa ni vigumu wanawake kukubali wanaume kwa urahisi. Wanaume nao wamebuni mbinu za kuwaendea wanawake kwa maneno matamu ya uongo ili kuwalainisha wakubali mambo yao. Ole wao wanawake wanachukulia maneno matamu ya wanaume kama injili takatifu,” asema Bw Kamemchi.

Misitari mitamu

Kulingana na wataalamu, watu wengi huamini misitari mitamu ndiyo kujua mapenzi au kupendwa.

” Huwa wanakosea. Misitari huwa inakusudiwa mtu katika mazingira aliyomo na lengo la anayeirushwa huwa ni ya wakati huo huo. Hata kama anatoa ahadi za siku zijazo, huwa ni hewa tu, ” asema Bi Ambani.

Hata hivyo, anakiri kwamba ikitolewa na mtu aliye makini kwa mapenzi hasa wale ambao tayari wameoana, huwa inaongeza ladha ya huba.

“Katika hali hii, misitari ninayozungumzia ni lugha tamu ya mtu kwa mkewe. Lugha ya heshima inayolenga kukuza mapenzi katika mtu na mchumba wake. Sio inayotolewa na wanaume watundu inayowafanya kuandamwa na vidosho ambao wanajuta baada ya kubaini walikuwa wakifuata mapenzi ya upepo, ” aeleza.

Anasema watu huwapoteza wachumba wazuri wasiowaahidi mambo makuu wakidai hawajui kurusha kutongoza au kuchangamsha vidosho.

“Heri mtu wa maneno machache anayejali kuliko mtu wa maneno mengi matatu asiyejali. Penzi ni zaidi ya kurusha roho, kuzuru maeneo tofauti na kudaganywa. Kabla ya kutoa roho na mwili wako kwa mtu anayekumiminia misitari mitamu akidai anakupenda, fikiria sana kipusa, “aeleza Bw Kamemchi.

Bi Ambani anasema jinsi hali ilivyo, wanawake wataendelea kuangukia mitego ya wanaume waliojawa na utundu kwa sababu ya tabia yao kupagawishwa kwa urahisi kwa maneno matamu ya kupenda starehe.